Serikali wilayani Geita imezitaka taasisi mbalimbali nchini kuendelea kujitolea kusaidia sekta ya elimu kama njia ya kuchangia maendeleo ya taifa.
Akizungumza wakati wa kupokea msaada wa madawati 100 yaliyotolewa na Benki ya Equity Tanzania kwa Shule ya Sekondari ya Wasichana Nyankumbu, Afisa Tarafa wa Wilaya ya Geita Moreen Komanya alisema hatua kama hiyo ni muhimu katika kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita
“Tunazihimiza taasisi nyingine pia zione umuhimu wa kusaidia sekta ya elimu kwa kuwa ndio msingi wa maendeleo ya taifa letu,” alisema Komanya
Meneja Mkuu wa Kitengo cha Biashara wa Equity Bank Tanzania Leah Ayoub alisema benki hiyo imekuwa ikijikita katika kuunga mkono jamii kwa maendeleo endelevu sambamba na huduma za kifedha
“Mbali na msaada huu wa madawati wenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 10, tumezindua pia tawi jipya la benki mjini Geita ili kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha na kuhakikisha ujumuishaji wa kifedha unakuwa na manufaa kwa jamii yote ya Watanzania,” alisema Ayoub
Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Nyankumbu Khadija Kayanda aliishukuru benki hiyo kwa msaada huo akibainisha kuwa utaboresha mazingira ya kujifunza na kuongeza ufaulu wa wanafunzi
“Madawati haya yatasaidia wanafunzi kupata sehemu ya kukaa na kusoma kwa bidii zaidi, na kama shule tunaahidi kuyatunza ili yaendelee kuwasaidia hata wanafunzi watakaokuja baadae,” alisema Kayanda
Nao wanafunzi wa shule hiyo akiwemo Agripina Elisha na Hilda Baton Sanga waliishukuru benki ya Equity kwa mchango huo na kuzitaka taasisi nyingine kuiga mfano huo
“Tunafurahi kuona taasisi za kifedha kama Equity si tu zinatoa huduma za kifedha bali pia zinaguswa na maendeleo ya elimu na jamii kwa ujumla,” alisema Agripina huku mwenzake Hilda akiongeza kuwa msaada kama huo unapaswa kusambazwa katika shule nyingine pia