Huu hapa utaratibu kuomba ufadhili masomo ya ubingwa bobezi wa afya

Dodoma. Serikali  imeendelea kuwekeza kwa kwenye sekta ya afya kupitia mpango wa ufadhili wa masomo Samia Health Super-Specialization Program, ambapo kwa mwaka wa fedha 2025/26  imetenga Sh9 bilioni kugharamia ufadhili wa mafunzo ya ubingwa na ubingwa bobezi kwa wataalamu wa afya.

Hayo yamebainishwa leo Alhamisi Agosti 21, 2025 na Waziri wa Afya, Jenista Mhagama, wakati akitoa taarifa kwa umma juu ya mpango huo kwa mwaka wa fedha 2025/26.

Waziri Mhagama amesema mpango huo unaosimamiwa na Wizara ya Afya utawezesha watumishi wa afya kupatiwa ufadhili wa masomo ya kibingwa kwa fani zenye uhitaji mkubwa ambapo  utahusisha ufadhili wa ada, nauli, posho ya utafiti na kujikimu kwa wanaosoma ndani na nje ya nchi, kwa viwango vilivyowekwa na Wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2025/26.

“Mpango huu maalumu unalenga kusomesha angalau wataalamu 300 wa afya kila mwaka katika fani mbalimbali zenye kipaumbele kwa seti, hatua inayolenga kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda nje ya nchi, kupunguza gharama kwa Serikali na wananchi na kuvutia tiba utalii,” amesema Waziri Mhagama.

Kuhusu dirisha la maombi Waziri Mhagama amefafanua kuwa limefunguliwa rasmi kuanzia Agosti 20, 2025 hadi Septemba 12, 2025 na maombi yanapaswa kuwasilishwa kwa njia ya kielektroniki pekee kupitia tovuti ya Wizara ya Afya.

Pia amesema vigezo vya kupata ufadhili vimeelezwa kwa kina katika tangazo rasmi kwenye tovuti ya Wizara ya Afya, miongoni mwao ni mwombaji kuwa mtumishi wa Serikali, raia wa Tanzania, awe amepata udahili kutoka chuo kinachotambuliwa na Serikali, na awe anakwenda kusomea fani zenye kipaumbele kulingana na uhitaji wa kituo chake cha kazi.

Mwisho Waziri Mhagama ametoa wito kwa waombaji wote kufuatilia tangazo lililopo katika tovuti ya wizara kwa anwani ya www.moh.go.tz kuwa makini na kuhakikisha wanatimiza masharti yaliyowekwa kwa niaba ya sekta hiyo.