Ifahamu kiundani teknolojia ya laini za eSIM na faida zake

Dar es Salaam. Kadiri teknolojia upande wa simu janja ikiendelea kushika kasi huenda wakati ujao, watumiaji wa simu hizo wakaachana ama kusahau kabisa matumizi ya laini za kadi zilizoeleka.

Hilo linawezekana kutokana na teknolojia ya simu kadi za kidijitali ijulikanayo kama eSIM (embedded SIM) ambayo inapatikana katika matoleo mapya ya simu za kisasa zinazoingia sokoni kila uchwao.

eSIM ni kadi ya SIM ya kidijitali ambayo imetengenezwa moja kwa moja kwenye kifaa, na kuondoa uhitaji wa kadi halisi ya plastiki tulizozizoea.

Mfano imezoeleka ukinunua simu, lazima uende kwa wakala akusajilie laini kisha ufungue simu yako uiweke ndani pengine wakati mwingine ikikaa vibaya, inaweza isisome, hivyo utapaswa kuitoa na kuiweka upya, lakini eSIM yenyewe unaunganisha laini ya kampuni unayotumia kidijitali.

Tofauti na SIM ya kawaida ambayo huunganishwa na kampuni ya simu na lazima ibadilishwe kwa kutoa na kuweka ya kampuni husika, eSIM ni chipu ndogo inayoweza kuwekwa kidijitali na taarifa za kampuni ya simu ya mtumiaji bila kuitoa.

Teknolojia hiyo inashika kasi wakati kwa sasa nchini Tanzania kwa mujibu wa ripoti za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), kuna laini za simu zaidi ya milioni 90.

Idadi kubwa ya laini hizi ni za simu za mkononi na laini za simu za mezani, ni chache sana.

Ongezeko hilo linaonyesha kasi kubwa ya kupanuka matumizi ya simu za mkononi nchini, ikichochewa na huduma nafuu, huduma za fedha kwa njia ya simu na kuenea kwa matumizi ya dijitali.

Teknolojia ya eSIM inafanya kazi sawa na SIM halisi yenyewe inakutambua kama mteja wa simu na kukuunganisha kwenye mtandao wa simu kwa ajili ya kupiga simu, kutuma ujumbe mfupi na data.

Hata hivyo, kwa kuwa eSIM imejengwa ndani, unaanza kwa kupakua profile kutoka kwa kampuni yako ya simu, mara nyingi kwa ku-scan msimbo wa QR au kupitia programu ya kampuni.

Ukirejea historia yake, eSIM wazo lake lilianza tangu mwaka 2010, Chama cha GSMA (Global System for Mobile Communications Association) kilianza kujadili wazo la teknolojia hiyo.

Ilipofika mwaka 2016, GSMA ilitoa rasmi vigezo vya eSIM kwa watumiaji huku kifaa cha kwanza kuitumia ilikuwa saa ya Samsung Gear S2 Classic 3G.

Mwaka 2017, Simu ya kwanza kutumia eSIM ilikuwa Google Pixel 2. Pia, 2018 kampuni ya Apple ilianza kutumia eSIM katika simu zao za iPhone XS, iPhone XS Max, na iPhone XR.

Kutokana na simu hizo kuanza kutumia eSIM ilisababisha matumizi yake kukua na kujulikana kwa watu wengi.

Ingawa simu nyingi mpya, saa janja, na baadhi ya kompyuta zina teknolojia ya eSIM, bado haipatikani kwenye vifaa vyote, hasa modeli za zamani.

Si simu zote zinazotumia eSIM, bali zenye sifa maalumu hasa zile za kisasa na za bei ya juu.

Teknolojia hii imejengwa ndani ya simu hivyo lazima kifaa hicho  kiwe na uwezo wa kuisapoti.

Kwa ujumla, simu zinazotumia eSIM mara nyingi ni za kampuni kubwa kama Apple, Samsung, na Google.

Mfano wa simu zinazotumia teknolojia hiyo ni Apple iPhone kuanzia iPhone XR, XS, na iPhone SE (2020/2022) na matoleo yote ya baada yake, yaani iPhone 11, 12, 13, 14, 15, na 16 ikihusisha na matoleo yao ya Pro, Pro Max, Mini, Plus).

Nchini Marekani, iPhone 14 na matoleo mengine mbele hayana kabisa sehemu ya kuweka SIM ya kawaida.

Samsung Galaxy hasa toleo la Galaxy S na Galaxy Z za matoleo ya karibuni kama Galaxy S20, S21, S22, S23, S24, na S25 (pamoja na matoleo yao ya FE, Plus, na Ultra) Galaxy Z Fold na Z Flip, Galaxy Note 20.

Ukiachana na Google Pixel 10 iliyozinduliwa jana Agosti 20, 2025 kutumia eSIM pekee kwa Marekani simu hizi ndio zinaongoza kwa matumizi ya eSIM na Pixel 10 nayo inatumia teknolojia hiyo.

Google Pixel 10 (pamoja na Pixel 10 Pro na 10 Pro XL) hutumia laini za eSIM pekee. Nje ya Marekani Google Pixel 10 inatumia laini ya kawaida na pia eSIM.

Google Pixel 3 na matoleo yote ya baada yake (hadi Pixel 9 na 9 Pro, 10) zinatumia eSIM.

Simu nyingine ni Huawei: P40, P40 Pro, Honor Magic4 Pro, Magic5 Pro, Oppo: Find X3 Pro, Find X5, Reno6 Pro 5G, Find N2 Flip, Motorola: Razr 5G.

Kompyuta mpakato na tableti baadhi yake pia zina uwezo wa eSIM, kama baadhi ya matoleo ya Microsoft Surface, Apple iPad  na vifaa vingine.

Jinsi ya kujua kama simu yako inatumia eSIM

Kwanza unatakiwa kupiga namba *#06#, kama simu yako ina uwezo wa eSIM, mbali na namba za IMEI basi utaona namba inayoitwa EID (eSIM Identifier).

Kama huoni namba za EID, basi tambua kuwa simu yako haina uwezo wa eSIM.

Aidha nenda kwenye Settings, mfano kwa simu za Android kama (Samsung/Google Pixel) nenda kwenye (Settings), kisha bonyeza Connections au Network & Internet), tafuta “SIM Card Manager au ‘Add mobile plan”.

Endapo utaona chaguo la “Add eSIM” au “Add mobile network”, basi simu yako ina uwezo wa eSIM.

Kwa iPhone nenda kwenye (Settings), kisha Cellular au Mobile Data, na utafute “Add eSIM” au “Add Data Plan” ikiwa ipo basi, simu yako inasapoti eSIM.

Kwanza eSIM hurahisisha kubadili kati ya mitandao ya simu au kuongeza laini ya pili kwa ajili ya biashara bila kulazimika kupata kadi mpya ya SIM halisi.

Unaweza kuhifadhi profiles nyingi za eSIM kwenye kifaa kimoja, ingawa kwa kawaida mbili tu ndizo zinaweza kutumika kwa wakati mmoja.

Pia, hata suala zima la usalama kwa sababu eSIM haiwezi kuondolewa kutoka kwenye kifaa au simu iliyoibwa, ni salama zaidi dhidi ya wizi wa kadi ya SIM au mashambulizi ya “SIM swap”.

Hii inafanya iwe vigumu kwa mwizi kutumia namba yako kwa shughuli za udanganyifu.

Aidha, eSIMs hupunguza taka za plastiki na uzalishaji wa kaboni unaohusishwa na utengenezaji, ufungaji, na usambazaji wa kadi za SIM za plastiki za kawaida.

Ukiwa na eSIM, huwezi tu kuhamisha kadi kutoka simu moja kwenda nyingine; unalazimika kupitia mchakato wa kuhamisha kidijitali, ambao wakati mwingine unaweza kuhitaji msaada wa kiufundi kutoka kwa kampuni yako ya simu.