Jalada tukio la mauaji ya mwanafunzi lapelekwa NPS

Arusha. Jalada la mashtaka kuhusu tuhuma za mauaji zinazowakabili wanafunzi 11 limepelekwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS) kwa hatua zaidi.

Wanafunzi hao wanatuhumiwa kwa mauaji ya Yohana Konki (17), mwanafunzi wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Qash.

NPS ndiyo ofisi yenye jukumu la kuamua watuhumiwa washtakiwe kwa kosa lipi. Yohana alizikwa jana, Agosti 20, 2025 katika Kijiji cha Tsamas, wilayani Babati Mkoa wa Manyara.

Anadaiwa kuuawa alfajiri ya Agosti 16, 2025 shuleni hapo, akidaiwa kuiba kishikwambi (iPad), tukio lililohusishwa na ramli chonganishi kutoka kwa mganga wa kienyeji ambaye bado anasakwa na Jeshi la Polisi mkoani Manyara.

Akizungumza na Mwananchi leo, Alhamisi Agosti 21, 2025, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Ahmed Makarani amesema jeshi hilo linaendelea kumsaka mganga huyo.

“Bado wale wanafunzi 11 tunawashikilia na tulikuwa tunakamilisha taratibu, tumepeleka jalada Ofisi ya Taifa ya Mashtaka. Tunasubiri maelekezo mengine. Mganga anaendelea kutafutwa, bado hatujampata,” amesema.

Akizungumza na Mwananchi Jumatatu, Agosti 18, 2025, Kamanda Makarani alisema jeshi hilo linaendelea na uchunguzi, ikiwemo kumsaka mganga anayedaiwa kukimbia na familia yake baada ya tukio hilo.

“Mganga alikimbia na familia yake na baadhi ya mizigo siku ileile baada ya kusikia ramli yake imeleta shida. Tunaendelea na uchunguzi wa tukio hili, ikiwamo kumtafuta na tunaamini tutampata,” alisema.

Alisema wanafunzi 11 wa shule wanashikiliwa wakidaiwa kumpiga mwenzao kwa tuhuma za wizi.

“Awali tuliwakamata wanafunzi 13, ila wawili tumewaondoa, wamebaki 11. Kati ya hao wawili, mmoja ushahidi unaonesha hakuwapo kabisa shuleni siku ya tukio,” alisema na kuongeza:

“Huyo mwingine wa pili tumemuondoa maana hata ushahidi wa wanafunzi wenzake unaonesha alikuwa anapita na pikipiki yake, ndipo akakuta tukio hilo. Na pikipiki yake ndiyo ilitumika kumbeba Yohana kumpeleka hospitali. Tunaangalia kwenye suala hili tutamuweka wapi, ila si mtuhumiwa kwa sasa.”

Elizabeth Konki, shangazi wa Yohana (marehemu), akizungumza na Mwananchi alieleza kusikitishwa na tukio hilo, akisema wamekatisha ndoto za kijana wake.

Hassan Juma, mmoja wa wanafunzi shuleni hapo, alidai Yohana alipigwa na wenzake kwa kumshambulia kwa fimbo mwilini kutokana na majibu ya mganga wa kienyeji.

Alidai walipotoka kwa mganga, walimuuliza iwapo amechukua kishikwambi. Alipokataa, ndipo walipoanza kumpiga.