Kanda ya ziwa yaongoza wanafunzi wanaoacha sekondari, wadau wataja suluhuhisho

Dar es Salaam. Takwimu mpya za Elimu ya Msingi (Best 2025) zinaonesha changamoto kubwa katika mfumo wa elimu nchini, hususani kwa wanafunzi wa sekondari katika Kanda ya Ziwa.

Ripoti hiyo iliyotolewa na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) inaonesha mwaka 2024 pekee, wanafunzi 100,109 wa sekondari walikatisha masomo, wakati mikoa ya kanda ya ziwa ikichangia takribani nusu ya hao.

Mkoa wa Mwanza uliongoza kwa wanafunzi (7,630) walioacha shule, Geita (7,498), Tabora (7,424), Dodoma (6,913), Kagera (6,618), Tanga (5,069) na Simiyu (4,793).

Hata hivyo, ikilinganishwa na miaka miwili iliyopita, wanafunzi wanaoacha sekondari wamepungua kwa zaidi ya asilimia 40. Mwaka 2023 walioacha shule walikuwa 148,337 na 136,313 kwa mwaka 2022.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Mei 23, 2024, akiwa bungeni jijini Dodoma, aliagiza wakuu wa mikoa, halmashauri na wakaguzi wa elimu kufuatilia wanafunzi waliotoroka masomo na kuhakikisha wanarudi shuleni, akisisitiza lengo la Serikali kuhakikisha angalau asilimia 95 ya watoto wanamaliza elimu ya msingi na sekondari.

Kauli hiyo ilifuatiwa na hoja ya aliyekuwa mbunge wa Sikonge, Joseph Kakunda, aliyelihoji bungeni mkakati wa Serikali kukabiliana na wimbi la wanafunzi wanaoacha shule.

Sababu za utoro, kurudia darasa

Ripoti ya Best Education 2025 ya Tamisemi pia imebainisha tatizo jingine linalokua kwa kasi la ongezeko la wanafunzi wanaorudia kidato cha pili.

Idadi hiyo imeongezeka kutoka wanafunzi 48,334 mwaka 2023 hadi 60,594 mwaka 2024, sawa na ongezeko la asilimia 25.36.

Wanafunzi wa kidato cha pili peke yao wameunda asilimia 94.41 ya wanafunzi wote waliolazimika kurudia kati ya kidato cha kwanza na cha nne.

Miongoni mwa sababu zinazotajwa ni kukosekana mazingira bora ya kujifunzia na kufundishia, changamoto ya lugha ya Kiingereza, uhaba wa vitabu, uchovu na kukosa motisha kwa walimu, pamoja na wazazi kushindwa kusimamia ipasavyo watoto wao.

Mdau wa elimu, Ochola Wayoga, amesema walimu wengi wamechoka na hawana morali ya kufundisha kwa bidii kutokana na changamoto za kimaisha, ikiwamo mishahara midogo na mikopo inayowabana.

“Huwezi kutegemea matokeo mazuri wakati walimu wako hawana motisha, wengine wapo tayari kuacha kazi endapo wakipata fursa nyingine,” amesema.

Amesema tatizo kubwa la wanafunzi kushindwa kufaulu linatokana na ukosefu wa ufuatiliaji.

“Mwanafunzi anaweza kuwa wa mwisho kidato cha kwanza, anaendelea kidato cha pili bila msaada wowote. Akifika kwenye mtihani ni wazi atashindwa,” amesema.

Mdau mwingine wa elimu, Muhanyi Nkoronko amesema kurudia darasa ni gharama kwa wazazi na Serikali, kwa kuwa rasilimali fedha hutumika mwaka mwingine wa masomo.

Amesisitiza walimu wafundishe kikamilifu na kuhakikisha mada zote zinamalizika kwa wakati ili kupunguza idadi ya wanaorudia. Pia ameonya juu ya athari za utoro, kwani wengi wanaorudia darasa huishia kuacha shule kabisa, wengine kuolewa mapema na kujiingiza kwenye vitendo vya uhalifu.

Ofisa Elimu Mkoa wa Mwanza, Martin Nkwabi, amesema wakati anaingia ofisini mwaka 2020 kiwango cha wanafunzi kuacha shule kilikuwa asilimia 21, lakini mikakati mbalimbali imesaidia kupunguza idadi hiyo hadi kufikia asilimia 3.2 mwaka huu.

“Mambo yaliyofanyika ni ujenzi wa miundombinu, kuongeza vitendea kazi, kuinua morali ya walimu na kuhamasisha wazazi kutoa chakula cha mchana shuleni. Pia tumeanzisha kamati za taaluma katika kata ambazo hufuatilia moja kwa moja utoro wa wanafunzi,” amesema.

Ofisa Elimu Mkoa wa Geita, Antony Mtweve, amesema wameanzisha utaratibu wa kuwawajibisha wazazi endapo watoto wao hawahudhurii shule kwa siku mbili au tatu mfululizo.

Vilevile, wanatoa huduma ya chakula na kuendeleza michezo kwa lengo la kuvutia wanafunzi wabaki shuleni.

Naye Ofisa Elimu Mkoa wa Kagera, Michael Ligola, amesema kila shule inahimizwa kuwa na shamba ili kuhakikisha wanafunzi wote wanakula. Pia, wameanzisha programu za kuwasaidia wanafunzi wa kike waliopata ujauzito kurejea shuleni baada ya kujifungua.

“Tunashirikiana na jamii kuwabana wazazi wanaowaacha watoto wao wachunge ng’ombe au kuwatumikisha kwenye ajira. Tunaelimisha madhara ya mimba za utotoni na ajira za mapema kwa wavulana,” amesema.

Mwongozo wa mwaka 2022 kuhusu urejeshaji wa wanafunzi waliokatisha masomo unaelekeza mwanafunzi anapaswa kurudi shuleni ndani ya kipindi cha miaka miwili tangu kuacha.

Unasisitiza uwepo wa kikao kati ya mzazi, uongozi wa shule na kamati ya shule ili kuweka mpango wa kumsaidia mwanafunzi husika.

Mwanafunzi hupewa nafasi ya kuamua kurejea shule aliyokuwa awali au kuhamia nyingine, huku akipatiwa huduma ya ushauri na unasihi. Shule na halmashauri zinatakiwa kuhakikisha wanafunzi wanarudi shuleni mwanzoni mwa mwaka mpya wa masomo na shule walizopangiwa ziwe karibu na makazi yao.

Hata hivyo, idadi kubwa ya wanaorudia kidato cha pili na changamoto za utoro bado zinaendelea kuathiri mfumo wa elimu na kuibua mjadala kuhusu wajibu wa walimu, wazazi, jamii na Serikali katika kuhakikisha kila mtoto anapata elimu bora na kumaliza masomo yake ipasavyo.