Miili ya watu wawili yaopolewa mgodini Shinyanga, idadi waliokufa yafikia saba

Shinyanga. Miili ya watu wawili waliofukiwa na kifusi kwenye mgodi uliopo katika Kijiji cha Mwongozo, halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, imeopolewa usiku wa kuamkia leo Agosti 21, 2025 na hivyo kufanya idadi ya waliopoteza maisha kwenye ajali hiyo kufikia saba.

Watu hao waliokuwa wakifanya kazi katika duara namba 20, linalomilikiwa na Kikundi cha Wachapakazi wilayani humo, wametambuliwa kuwa ni Japhet Massanja (30) na Chembanya Makenzi (25).

Ajali hiyo ilitokea Agosti 11, 2025 wakati maduara ya mgodi huo yakikarabatiwa kabla ya kusababisha mgodi huo kutitia na kuwafukia watu 25.

Watu watatu waliokolewa wakiwa hai na kukimbizwa hospitalini kwa huduma ya kwanza, wawili wameruhusiwa lakini mmoja alipewa rufaa ya kwenda Bugando, Mwanza kwa ajili ya matibabu zaidi.


Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu leo Agosti 21, 2025, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita amethibitisha kutolewa kwa miili ya watu hao waliokuwa wamefukiwa ardhi, hivyo wamebaki watu 15 ambao bado juhudi za kuwatafuta zinaendelea.

“Watu wawili wametolewa usiku wa kuamkia leo wakiwa wamepoteza maisha, idadi ya watu waliotolewa imefika 10, saba wakiwa wamekufa na watatu wakiwa hai, bado watu 15 ambao juhudi za kuwatafuta zinaendelea,” amesema Mhita.

Agosti 13, 2025, mtu mmoja aliokolewa akiwa ni majeruhi, alipelekwa hospitalini lakini juhudi za madaktari hazikufua dafu kwani majeruhi huyo alifariki wakati anapatiwa matibabu, juhudi za kuokoa ziliendelea na Agosti 15 mwili wa mtu mmoja uliopolewa.

Agosti 16, 2025, watu wawili waligundulika walipo chini ya ardhini na Agosti 17, 2025, watu hao walitolewa wakiwa wamefariki dunia. Agosti 19, 2025, mtu mmoja alitolewa akiwa amepoteza maisha.


Hadi sasa watu kumi wametolewa huku watatu wakiwa hai na saba wakiwa wamefariki, juhudi za kuendelea kuwatoa wengine 15 zinaendelea kwa kasi kwa kutumia mashine za utambuzi wa ardhini kujua maeneo waliopo.