Mkandala awindwa Coastal Union | Mwanaspoti

UONGOZI wa Coastal Union uko katika mazungumzo ya kumsajili aliyekuwa nyota wa Kagera Sugar FC, Cleophace Mkandala baada ya kiungo huyo kumaliza mkataba, huku kukiwa hakuna mazungumzo ya kuongeza mwingine mpya wa kukichezea pia kikosi hicho.

Nyota huyo wa zamani wa matajiri wa Jiji la Dar es Salaam Azam FC, ameamua kutafuta changamoto sehemu nyingine baada ya Kagera Sugar kushuka daraja kutoka Ligi Kuu hadi Championship, ambapo kwa sasa Coastal Union inafanya mazungumzo naye.

Taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata, zinaeleza Mkandala yupo hatua za mwisho za kujiunga na kikosi hicho cha ‘Wagosi wa Kaya’ kwa mkataba wa mwaka mmoja wenye kipengele cha kuongeza mwingine, huku akiwa amefika Tanga kukamilisha dili hilo.

“Mkandala tayari ameungana na Coastal Union ambayo imeweka kambi ya maandalizi ya msimu mpya ‘Pre Season’ hapa Pangani mjini Tanga, mazungumzo yamefikia sehemu nzuri na muda wowote kuanzia sasa atasaini mkataba huo,” kilisema chanzo hicho.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Habari na Mawasiliano wa Coastal Union, Abbas Elsabri alisema baada ya kukamilisha pia taratibu zote za kutambulisha benchi jipya la ufundi la timu hiyo, kwa sasa wanajiandaa kutangaza nyota wapya kikosini.

“Siwezi kusema ni mchezaji gani tuliyemsajili kwa sasa lakini niwahakikishie mashabiki zetu watarajie mambo mazuri kwa msimu ujao, tutatambulisha wachezaji ambao kila mmoja wetu atakiri tumejipanga kuleta ushindani zaidi,” alisema Elsabri.

Hata hivyo, licha ya kauli ya Elsabri, ila Mwanaspoti linatambua Mkandala anakaribia kujiunga na kikosi hicho, akiungana na nyota mwenzake, Jofrey Manyasi ambao wote msimu uliopita wa 2024-2025, waliitumikia Kagera Sugar iliyoshuka daraja.

Nyota wengine waliosajiliwa na kikosi hicho ni Ally Ramadhan Kagawa (Geita Gold), Mahmoud Haji Mkonga ‘Aguero’ (Mlandege, Athumani Masumbuko ‘Makambo Jr’ kutoka Viktoria 06 Griesheim ya Ujerumani na Adam Salamba kutokea Branes ya Libya.