Moto wateketeza nyumba ya mchungaji Tabora

Tabora. Moto umezuka na kuteketeza nyumba yenye vyumba tisa ambayo anaishi mmoja kati ya wachungaji wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Tabora iliyopo Barabara ya Kilimatinde, Kata ya Cheyo, Manispaa ya Tabora.

Katika ajali hiyo ya moto iliyotokea usiku wa jana Jumatano, Agosti 20, 2025, hakuna mtu aliyepoteza maisha lakini mali mbalimbali zilizokuwamo zimeteketea.

Mchungaji Amosi Chidemi ambaye alikuwa anaishi katika nyumba hiyo amesema saa moja usiku wakati akiwa sebuleni na familia yake wakaona moshi unajaa ndani na baada ya kwenda kuangalia unapotokea moshi wakaona moto tayari umeshatanda katika baadhi ya vyumba.

Amesema yeye pamoja na familia yake wametoka salama lakini hajui nini ambacho kimeokolewa mpaka kwani majirani walianza uokoaji wakati tayari moto umeshakuwa mkubwa.

“Wakati tumekaa sebuleni, tumemaliza kula chakula tukawa tunaongea, tukashangaa moshi unaingia sebuleni.

Nikatoka ili niangalie moshi unatoka wapi ndio nikakuta ile pazia ya kwenye korido ndio imeshatanda moto ukiwa ni mkali kabisa, mke wangu akanivuta kwamba tutoke nje kupitia mlango mwingine, ndio tukanusurika wote,” amesema.

Meshaki Stanford dereva bodaboda Manispaa ya Tabora ambaye ni shuhuda wa tukio hilo, amesema wakati wamekaa kijiweni wakisubiri abiria wakaona moshi mkubwa juu na watu wanalia.

“Tumekuja hapa tukakuta moto ni mkubwa ndio nikachukua simu nikawapigia Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kuwa nilijua kabisa ule moto sio rahisi kuuzima sisi wenyewe, tunashukuru wamewahi kufika na kuuzima moto,” amesema.

Shuhuda mwingine, Moses Mathias amesema amekuta moto umetanda hata kuingia ndani kuokoa vitu ilibidi kuvunja mlango japo vitu vilivyookolewa ni vichache.

“Sisi tumepambana kuokoa vitu japo hatukufanikiwa sana kutokana na moto kuwa mkubwa vitu vingi vilishaungua na moto,” amebainisha.

Kwa upande wake, ofisa kutoka Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Tabora, Gabriel Masamalo amesema vyumba vitano kati ya tisa vya  nyumba hiyo vimeungua moto huku akibainisha wamepigiwa simu wakati ambapo moto umeshakuwa mkubwa.

“Wananchi niwasisitize  kuwa moto unapotokea wapige simu kwanza kwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ndipo waendelee na juhudi zao badala ya kuanza jitihada zao halafu wakikwama ndio wanakumbuka kupiga simu zimamoto jambo ambalo linapelekea mara nyingi moto kuwa mkubwa na kusababisha hasara,” amesisitiza.

Amesema  ni vitu vichache vilivyoolewa ikiwemo luninga, pikipiki na makochi, vingine ni vitu vidogo vidogo tu.

“Ni vichache vipo hapa vilivyookolewa jambo la muhimu ni kwamba watu wote wamenusurika wako salama,” amesema.