Profesa Mbarawa ataka tafiti zilete tija sekta ya usafirishaji

Dar es Salaam. Ili kuongeza ufanisi wa utoaji huduna katika sekta ya usafiri, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa ametaka tafiti zinazolenga kuleta suluhisho katika sekta husika, zitafsiriwe ili kuchochea matokeo chanya.

Ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Agosti 21, 2025 wakati akifungua mkutano wa tatu wa kimataifa wa usafiri na usafirishaji uliofanyika jijini hapa na kuwakutanisha wadau wa sekta hiyo kutoka maeneo mbalimbali ulioandaliwa na Chuo cha Usafirishaji (NIT).

Kufunguliwa kwa mkutano huo kumeenda sambamba na kuzinduliwa kwa maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Chuo cha NIT.

Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa



Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano huo,  Profesa Mbarawa amesema Serikali inaendelea na maboresho mbalimbali, hivyo ni vyema tafiti zilizopo zitumike kusaidia kuboresha huduma.

“Tunafanya tafiti kwenye maeneo mbalimbali, sekta ya uchukuzi nayo kuna tafiti ambazo zinafanyika kama zitaweza kubadilishwa na kufanywa kwa vitendo, zitaweza kutatua matatizo mengi yanayoikabili sekta ya uchukuzi,” amesema Profesa Mbarawa.

Ametoa rai hiyo wakati ambao Serikali inaendelea kuhakikisha uwekezaji katika miundombinu unaenda sambamba na uzalishaji wa rasilimali watu wanaohitajika.

Katika kulitambua hilo, Serikali imewezesha NIT kutayarisha wataalamu kwa ajili ya sekta ya usafiri na usafirishaji huku akitolea mfano wa hapo awali marubani walipokuwa wakilazimika kwenda kusoma nje ya nchi.

“Leo hii tunazalisha kozi maalumu ambayo itafundisha vijana wa Tanzania kuwa marubani. Kozi hii ada yake ni kati ya Sh100 milioni hadi Sh150 milioni, lakini Tanzania itafanywa kwa bei rahisi ikiwa na viwango vya kimataifa,” amesema waziri huyo.

Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa.



Akizungumzie eneo la reli, Profesa Mbarawa amesema vyuo viwili vitajengwa, kimoja kitakuwa chini ya Shirika la Reli Tanzania huku bandari nao wakiwa na Chuo cha Bahari.

“Na hili matunda yake yameanza kuonekana kwa sababu kwa miaka mingi iliyopita, NIT wamefundisha wanafunzi wengi na kila eneo ulilopita utawakauta wakifanya shughuli za uchukuzi iwe ni serikalini au sekta binafsi,” amesema Profesa Mbarawa.

Awali, akizungumza, Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Profesa Ulingeta Mbamba amesema mkutano huo unadhihirisha dhamira ya taasisi katika kuunga mkono mageuzi ambayo serikali inaendelea kuyatekeleza katika sekta ya usafirishaji.

Amesema mageuzi hayo yameongeza mahitaji ya wataalamu wenye ujuzi wa hali ya juu hapa Tanzania na katika jamii.

“Katika muktadha huu, mkutano huu unakuwa jukwaa la kimkakati kuhakikisha kuwa Taasisi inaendelea kuwa muhimu katika kuiunga mkono serikali kushughulikia changamoto na kuchangamkia fursa zilizopo katika sekta hii kupitia suluhisho bunifu na zenye msingi wa tafiti,” amesema Profesa Mbamba.

Amesema mkutano wa mwaka huu unafanyika wakati NIT inajivunia kutimiza miaka 50 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1975.

Amesema mafanikio yanayosherehekewa yamewezekana kwa jitihada za wadau wengi, huku serikali ikiwa katika nafasi ya msingi.

“Tukio hili ni ushahidi wa msaada endelevu wa serikali na dhamira yake thabiti kwa ukuaji wa Taasisi pamoja na sekta ya usafirishaji na ninatoa shukrani za dhati kwa watu wote, kampuni na taasisi ambazo zimewezesha tukio hili kufanyika,” amesema.