Iringa. Kongamano la Iringa Business Connect limefunguliwa rasmi leo Alhamisi Agosti 21, 2025 katika Viwanja vya Kichangani, Manispaa ya Iringa, likishirikisha wafanyabiashara, wajasiriamali, wawekezaji na taasisi mbalimbali zinazotoa huduma kwa wafanyabiashara.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James amewataka wafanyabiashara kutumia vyema kongamano hilo kutangaza bidhaa na huduma zao ili kuongeza wigo wa soko.
RC James pia amesisitiza umuhimu wa kufanya biashara kwa weledi, kwa faida na kwa kufuata taratibu ili waweze kufikia mafanikio endelevu.
”Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi na Wafanyabiashara wote ili kuhakikisha mazingira bora ya kufanya biashara yanaimarishwa kila siku,” amesema RC James.
Mwenyekiti wa kongamano hilo ambaye pia ni Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Iringa, Peter Jackson amesema kuwa kongamano hilo linalenga kutoa fursa kwa wadau wa biashara kuunganishwa na taasisi za serikali na taasisi za fedha.
Jackson amesema kwa siku ya kwanza jana Agosti 20, 2025 mpaka leo Agosti 21, 2025 ikiwa ni siku ya pili ya kongamano ni zaidi ya wafanyabiashara 50 wameshiriki na matarajio ni kufikia zaidi ya wananchi 5,000 ifikapo mwisho wa kongamano hilo Agosti 22, 2025.
Ameeleza kuwa kongamano hilo limeandaliwa mahususi kwa lengo la kuchochea ukuaji wa uchumi kwa kuwaunganisha wafanyabiashara wakubwa na wadogo na kuwapa elimu kuhusu namna ya kurasimisha biashara, kupata mikopo, na kuongeza faida kwenye shughuli zao.
Katika mahojiano maalum na Mwananchi Digital, mfanyabiashara wa batiki kutoka Manispaa ya Iringa, Anna Mocha amesema kongamano hilo ni fursa adhimu kwa wafanyabiashara kuonyesha bidhaa zao na kupata mitandao mipya ya kibiashara.
“Maonyesho haya yametupa nafasi si tu ya kuuza bali kujifunza kutoka kwa wajasiriamali wengine na taasisi kama TRA kuhusu umuhimu wa urasimishaji wa biashara,” amesema Anna.
Kwa upande mwingine, baadhi ya wafanyabiashara ambao hawajarasimisha biashara zao wamepata fursa ya kupewa maelezo ya moja kwa moja na watendaji wa TRA kuhusu umuhimu wa kuwa rasmi kibiashara.
Kongamano hilo pia limehusisha benki, taasisi za kifedha, halmashauri na wadau wa maendeleo ambao wanatoa elimu, huduma na fursa mbalimbali kwa wafanyabiashara waliopo kwenye maonesho hayo.
Wajasiriamali kutoka sekta mbalimbali kama ushonaji, usindikaji wa vyakula, teknolojia, utalii na kilimo pia wameonyesha bidhaa na huduma zao, wakipata fursa ya kuunganishwa na masoko mapya.
Waandaaji wamesema maonyesho hayo yataendelea hadi Agosti 22, 2025 na yatakuwa na vipindi vya elimu ya biashara, majadiliano ya kitaalamu na fursa za mafunzo kwa vijana na wajasiriamali chipukizi.
Wananchi waliotembelea kongamano hilo wamepongeza uandaaji wake wakisema limekuwa fursa nzuri ya kupata elimu ya biashara na kuona bidhaa mbalimbali zinazotengenezwa na wajasiriamali wa ndani.
Mmoja wa wananchi, Neema Kalinga, mkazi wa Ipogolo amesema,
“Nimejifunza mambo mengi kuhusu namna ya kurasimisha biashara na pia nimepata mawasiliano ya taasisi muhimu za kifedha,”amesema.
Wengine wamesema kuwa kongamano hilo limetoa mwanga kwa wafanyabiashara wadogo ambao mara nyingi hukosa taarifa kuhusu huduma zinazopatikana serikalini na kwa taasisi binafsi.
Wananchi hao wameiomba Serikali kuhakikisha makongamano kama haya yanafanyika mara kwa mara, na pia kuyafikisha katika kata na vijiji ili kuwafikia wananchi wengi zaidi.
Kwa ujumla, kongamano la Iringa Business Connect limeonyesha taswira mpya ya mshikamano kati ya sekta binafsi na ya umma katika kuinua uchumi wa Mkoa wa Iringa na kuwahamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi.