RC SENDIGA AWEKA JIWE LA MSINGI SOKO LA MADINI MIRERANI

Na Mwandishi wetu, Mirerani

MKUU wa mkoa wa Manyara, Queen Sendiga amemuagiza mkandarasi aliyejenga soko la madini ya vito Tanzanite Trading centre mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro kukamilisha mradi huo kwa wakati.

Sendiga ameyasema hayo wakati akiweka jiwe la msingi la jengo la sakafu tano la soko la madini ya vito linalojengwa na shirika la nyumba la Taifa (NHC).

Sendiga amewataka NHC kuhakikisha kuwa wanakamilisha jengo hilo ili ifikapo Septemba 15 mwaka 2025 shughuli za uuzaji na ununuzi zianze kufanyika.

Ameeleza kwamba soko hilo la sakafu tano likikamilika litaongeza thamani ya eneo hilo hivyo wana Simanjiro, wana Manyara na watanzania kwa ujumla wachangamkie fursa hiyo.

“Viongozi wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro natoa maelekezo kwenu hakikisheni viwanja vilivyopo jirani vinatolewa bila urasimu na watu wachangamke kujenga,” ameagiza Sendiga.

Msimamizi wa ujenzi wa soko hilo kutoka shirika la nyumba la taifa NHC, Anna Akyoo amesema Sh5. bilioni zimetumika kwa ajili ya ujenzi wake.

Akyoo amesema mradi huo umefikia asilimia 98 na watahakikisha wanatekeleza maelezo ya mkuu huyo wa mkoa katika kukamilisha ujenzi huo.

Amesema mkataba wao umewaelekeza wamalize sakafu mbili ili sakafu tatu za jengo hilo zilizobakia zikamilishwe na halmashauri ya wilaya ya Simanjiro.

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro Gracian Makota amesema wanakila sababu ya kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutenga fedha hizo wa ujenzi wa soko hilo.

“Miradi ya maendeleo ni mingi hapa nchini ila wana Simanjiro tunashkuuru na pia mkuu wa mkoa amekuwa mwepesi kutusemea vyema wana Simanjiro juu ya jengo hili,” amesema Makota.

Mwenyekiti wa chama cha wachimbaji madini mkoa wa Manyara, (MAREMA) Elisha Mnyawi amesema hivi sasa wamepata eneo sahihi la kuuza madini yao na watalipa kodi kwa uhakika.

Mnyawi ameeleza kupitia jengo hilo wachimbaji madini hasa ya Tanzanite wamepata eneo zuri la kuuza madini yao bila kikwazo.

Makamu Mwenyekiti wa chama cha wachimbaji madini wanawake Tanzania (TAWOMA) Rachel Njau amesema ilikuwa hamu yao madini ya Tanzanite yanayopatikana pekee nchini kupata soko la uhakika.

Mmoja wa wafanyabishara hao Joyce Mkilanya ameeleza kwamba wanawake wauza madini wameishukuru serikali kwa kufanikisha ujenzi huo kwani itawarahisishia biashara zao.