:::::::
Serikali imeendelea na jitihada za kuhakikisha vijana wote wanapata elimu stahiki kwa kuwaandalia mdahalo maalum waliopo nje ya mfumo rasmi, lengo likiwa ni kusikiliza maoni yao kuhusu ujuzi wanaohitaji ili waweze kujiajiri na kushiriki kikamilifu kwenye uchumi wa nchi.
Mdahalo huo umefanyika Agosti 21, 2025 katika Ukumbi wa Maktaba mpya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na umehudhuriwa na vijana kutoka maeneo mbalimbali pamoja na wadau wa elimu.
Akizungumza katika ufunguzi wa mdahalo huo, Kamishna wa Elimu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Lyabwene Mtahabwa amesema mageuzi ya elimu yanayotekelezwa hivi sasa yanazingatia maoni ya vijana ili kuhakikisha yanajibu mahitaji ya sasa na baadaye.
“Tunapitia Sera ya Elimu na Mafunzo ya 2014 (Toleo la 2023) kwa lengo la kuhakikisha elimu nje ya mfumo rasmi inawapa vijana ujuzi wa kujitegemea, maadili na maarifa yanayokubalika kitaifa na kimataifa,” alisema Dkt. Mtahabwa.
Baadhi ya vijana walioshiriki, akiwemo Jeremia Pius kutoka Shule ya Sekondari Kijitonyama, walisema mdahalo huo umewasaidia kutambua nafasi yao katika jamii na kuwapa mwanga wa kimaisha. “Tumejifunza stadi za maisha na namna ya kujiamini,” alisema.
Mariam Fidelis kutoka Chuo cha Ufundi Stadi (VTC) alisema amejifunza umuhimu wa kujitambua na kuepuka makundi hatarishi, ili aweze kuwa mfano wa kuigwa kwa vijana wenzake.
Kwa upande wake, mwakilishi wa UNICEF, Simone Vis, alisema taasisi hiyo inajivunia kushirikiana na Serikali kwenye safari ya mageuzi ya elimu kwa kuwawezesha vijana, hususan wasichana, kupata fursa za elimu na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii.
Mdahalo huo ni sehemu ya mchakato unaoendelea wa kupitia miongozo ya utekelezaji wa sera, ili kuhakikisha elimu inamkomboa Mtanzania na kumwezesha kushindana ndani na nje ya mipaka ya nchi.
PICHA ZOTE NA JAMES SALVATORY TORCH MEDIA