Serikali yawezesha upasuaji watu 10, wengine 621 wafanyiwa vipimo

Mbeya. Kambi ya madaktari bingwa wa upasuaji katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya imefanikiwa kufanya upasuaji wa mgongo kwa watu 10 kati 602 waliofika kliniki kufanyiwa uchunguzi wa awali.

Idadi hiyo ilihusisha makundi mbalimbali ya wananachi waliohudhuria kliniki kufanyiwa uchunguzi ambapo baadhi yao walibainika chanzo cha matatizo ya mgongo ni saratani, ajali, udhoofu wa viungo na  nyinginezo.

Awali, kambi hiyo ilianza  Agosti 5 mpaka 11 mwaka huu ikihusisha wagonjwa kutoka mikoa ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini.

Akizungumza na Mwananchi  Digital  leo Jumatano Agosti 21, 2025 Daktari Bingwa wa Mifupa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya,  Dk Mulokozi Mutagwaba amesema waliofanyiwa  vipimo vya uchunguzi baadhi yao  wamebainika na matatizo ya  saratani, udhaifu wa viungo kutokana na umri mkubwa hususani ajali.


Dalili za matatizo ya mgongo

 Dk Mutagwaba ametaja miongoni mwa  dalili ni pamoja na maumivu ya viungo, mgongo na kwamba ni vyema jamii ikiona dalili hizo kuwahi kupata vipimo na ushauri  wa kitaalamu kabla ya kufikia hatua ya upasuaji.

“Zipo sababu mbalimbali uchangia matatizo ya mgongo hususani umri mkubwa, udhoofu viungo, saratani na ajali mbalimbali zikiwepo za barabarani ambazo madhara,” amesema.

Amesema kutokana na changamoto  hiyo jamii iwe na utaratibu  wa kupima afya mara kwa mara hususani makundi ya vijana na wazee ili kukabiliana na athari za matatizo  ya mgongo.

“Kimsingi kwa sasa huduma za upasuaji zinapatikana katika Hospitali yetu ya kanda tofauti na miaka ya nyuma mgonjwa alilazimika kusafirishwa kwenda  Muhimbili  jambo ambalo ulazimika kutumia gharama kubwa,”amesema.

Katika hatua nyingine amesema kitendo cha Serikali ya awamu ya sita kufanya uwekezaji mkubwa wa miundombinu hususani uwepo wa vifaa tiba vya kisasa kumesaidia jamii kupata huduma maeneo ya jirani.


“Kwa sasa huduma za kibingwa zinapatikana katika hospitali ya Kanda hivyo wananchi watumie fursa hiyo kufika kupata huduma  mbalimbali za kibingwa bobezi,” amesema.

Mkazi wa Mkoa wa Njombe, Steven Aloyce ambaye alimpeleka mgonjwa kupata matibabu ya mgongo amesema wameona namna huduma zilivyoboreshwa na kwamba awali walikuwa wakienda Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya matibabu zaidi ya kiuchunguzi.

“Nimefurahia huduma za uchunguzi wa matibabu hususani kwa wazee  ni tofauti na miaka ya nyuma lakini tunapaswa kuishukuru Serikali kwa uwekezaji huu mkubwa kwa kusogeza huduma za kibingwa bobezi,” amesema.