Sharon atakumbukwa kwa umahiri, weledi, azikwa nyumbani kwao Pugu

Dar es Salaam. Safari ya siku 19,154 za maisha ya mwanahabari Sharon Sauwa imehitimishwa leo baada ya maziko yake yaliyofanyika katika makaburi ya familia yaliyopo nyumbani kwao Pugu Mwakanga, jijini Dar es Salaam.

Sharon, aliyekuwa mwandishi wa habari wa Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL) akiripoti kutoka mkoani Dodoma, alifariki dunia alfajiri ya Agosti 19, 2025, wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili baada ya kuugua kwa takribani wiki mbili.

Mtoto wa marehemu Sharon Sauwa,Brighton Nandi akitoa heshima za mwisho wakati wa kuaga mwili wa mama yake, katika kanisa la Katoliki Pugu. Picha na Michael Matemanga



Mamia ya waombolezaji walioungana katika misa ya maziko iliyofanyika katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Francis, Pugu, Dar es Salaam, wamesema tasnia ya habari imepata pigo kufuatia kifo cha mwanahabari huyo.

Wengi wamemtaja kuwa alikuwa na weledi wa hali ya juu katika utekelezaji wa majukumu yake.


Akitoa salamu zake za pole, Waziri wa Mawasiliano, Habari na Teknolojia, Jerry Silaa, amemtaja Sharon kama miongoni mwa waandishi mahiri waliofanya kazi zao kwa weledi.

Amesema katika kipindi chote alichokuwa bungeni, Sharon alionesha umahiri mkubwa katika kuripoti habari za Bunge na kuwa daraja kati ya wananchi na Serikali.


“Kila mbunge au aliyewahi kuwa mbunge angepata nafasi ya kusema, angesema namna alivyokuwa rafiki, ndugu na mama. Alikuwa mwandishi mwenye weledi, akiwa na jambo atakuuliza kwa unyenyekevu. Nitoe pole kwa tasnia ya habari,” amesema Silaa, ambaye pia alitoa salamu za pole kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi.

Akitoa salamu za rambirambi, Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Rosalynn Mndolwa-Mworia, amemtaja Sharon kuwa alikuwa mlezi wa waandishi wengi wa habari ndani na nje ya kampuni hiyo.


“Katika kipindi chote cha miaka 13, Sharon alikuwa mwalimu kwa wenzake. Tangu kutokea kifo chake, salamu tulizozipata zimedhihirisha aliishi vyema na wenzake. Leo tumejumuika kumsindikiza katika safari yake ya mwisho, tukimuombea afike salama, tukijua ipo siku tutakutana,” amesema Rosalynn.

Kwa upande wake, Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali mstaafu, Ludovick Utouh, amemtaja Sharon kwamba alikuwa mwandishi makini aliyekuwa akiandika kile anachokiamini bila kupindisha ukweli.

“Alikuwa mwandishi anayeandika kitu anachoamini, alielimisha Watanzania wengi. Kilichotokea kwa Sharon ni wakati wake umefika, tuendelee kumuombea.  Mwenyezi Mungu ana haki ya kuvuna shambani kwake,” amesema Utouh.

Mtoto wa marehemu Sharon Sauwa, Brighton Nandi akiaga mwili wa mama yake uliohifadhiwa kwenye jeneza, ulipokuwa ukishushwa kaburini, Pugu. Picha na Michael Matemanga



Mbunge mstaafu, Joseph Selasini, amesema hakuna mwanasiasa ambaye hajaguswa na maisha ya Sharon kwa kuwa alitumia kalamu yake vyema katika kuripoti habari za siasa na Bunge.


“Hakuna mwanasiasa ambaye hakuguswa na Sharon. Alifanya kazi kubwa ya kufundisha na kuelimisha Taifa hili. Leo tunamshukuru Mungu kwa zawadi ya maisha yake.

“Alikuwa mama na dada mwema, akishirikiana na watu wote. Alikuwa mshauri mzuri, huwezi kumuona akiwa na uchungu hata akiwa na tatizo kubwa kiasi gani,” amesema Selasini, ambaye pia ni kaka yake kiukoo.


Amesema Sharon alifuata tabia za wazazi wake kupenda kusali. “Niwakumbushe waandishi wa habari, Sharon alishawahi kupata kesi kwa sababu ya kazi yake, lakini sijui iliisha namna gani. Nilikuwa nakutana naye, ananiambia ‘kaka usisahau kuniombea, twende tukasali.’ Ama kwa hakika tunapaswa kila siku kuandaa vifo vyetu, hakuna kifo cha ghafla.”

Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, Meneja wa Dawasa Ukonga, Mhandisi Honest Makoyi, amesema licha ya Sharon kuwa rafiki na dada kwa waziri huyo, alikuwa mtu wake wa karibu katika kazi.


Mwakilishi wa Klabu ya Waandishi wa Habari Dodoma (Dodoma Press Club), Mussa Yusufu, amesema Sharon amekuwa katika klabu hiyo kwa takribani miaka 15.

Amemwelezea kama mwandishi mwenye kipaji cha pekee, ambaye licha ya kipaji chake aliwashirikisha wengi waliopata wasaa wa kukutana naye.

“Alizichakata kwa weledi habari za Bunge la Tanzania. Tunafahamu zilikuwa ngumu, lakini alizichakata kwa umahiri na kuweza kueleweka na wananchi wa kawaida.

“Sharon hakuwa mwalimu pekee, bali alikuwa mama wa kutupatia fursa na mawazo chanya sisi vijana kuhusu kazi na maisha,” amesema Mussa.

Sharon alizaliwa Machi 10, 1973, na safari yake ya elimu alipitia shule mbalimbali jijini Dar es Salaam kabla ya kujiunga na chuo cha uandishi wa habari.


Mwaka 2002 alihitimu diploma ya uandishi wa habari na kuanza kazi kama mwandishi katika Kampuni ya The Guardian Limited, akiandikia gazeti la Nipashe, kabla ya mwaka 2013 kujiunga na Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd.