Dar es Salaam. Pacha walioungana, Abby na Brittany Hensel wametumia zaidi ya miaka 30 ya maisha yao wakiishi kwa mshikamano wa kipekee, tofauti kabisa na pacha wengine unaowafahamu. Abby alifunga ndoa na mwanajeshi mstaafu wa Jeshi la Marekani, Joshua Bowling mwaka 2021, huku dada yake Brittany akibaki hana mwenzi.
Wiki iliyopita, wawili hao wenye umri wa miaka 35 kutoka Minnesota walionekana wakiwa wamebeba mtoto mchanga, jambo lililoibua tetesi kwamba huenda wameanza kutimiza ndoto yao ya siku moja kuwa wazazi.
Pacha hao walizaliwa mwaka 1990 wakiwa na hali nadra inayoitwa dicephalic parapagus, ambapo mwili ni mmoja lakini kila mmoja ana kichwa chake. Waliwavutia mamilioni ya watu duniani baada ya kuonekana kwenye kipindi cha Oprah Winfrey na jarida la Life mwaka 1996.

Ingawa walipokuwa wachanga madaktari walitabiri wasingeweza kuishi usiku wa kwanza, walipingana na nadharia hiyo na hadi leo wanaendelea kuishi maisha ya ajabu yanayowashangaza wengi.
Ndoa na maisha ya kila siku
Mnamo 2021, Abby aliolewa na Joshua, ambaye tayari ana binti aitwaye Isabella kutokana na ndoa yake ya awali. Cheti cha ndoa kilichoibuliwa na vyombo vya habari kilithibitisha kwamba ni Abby pekee aliyeolewa, na siyo Brittany, jambo lililozua mjadala kuhusu hali ya kisheria ya uhusiano huo.
Baadaye, Joshua alionekana kuchochea uvumi wa kuwa na mtoto aliposhiriki picha ya vifaa vya mtoto wachanga kwenye mtandao wa X. Hali hii imezua maswali mengi kuhusu iwapo kweli pacha hao wamepata mtoto, au walitumia njia nyingine kama vile kuasili au kupitia mama mbadala.
Abby na Brittany ni kati ya pacha wachache zaidi walioungana ambao waliweza kufikia utu uzima wakiwa na afya nzuri. Wamekuwa wakifahamika kupitia kipindi chao cha televisheni kinachoonyesha maisha yao ya kila siku, kuanzia kuhitimu shule ya sekondari, kutafuta ajira, hadi kufundisha hisabati katika shule ya msingi huko Minnesota.
Mama yao, Patty, aliwahi kueleza kupitia makala ya kipindi cha televisheni kuwa pacha hao walitamani kupata watoto, akibainisha kwamba viungo vyao vya uzazi vinafanya kazi. Brittany naye alisema wazi: “Ndiyo, siku moja tutakuwa mama.”
Kwa mujibu wa wataalamu wa tiba, pacha walioungana ni nadra sana, mmoja hutokea kati ya watoto 40,000 wanaozaliwa, na ni asilimia moja pekee huishi zaidi ya mwaka mmoja. Abby na Brittany wanashirikiana viungo vingi vya mwili, ikiwemo ini, mfumo wa damu na viungo vya uzazi, lakini kila mmoja ana moyo wake, tumbo lake na kichwa chake.
Cha kushangaza zaidi ni kwamba licha ya kila mmoja kutoweza kuhisi upande wa mwili unaomilikiwa na mwenzake, miili yao hujitokeza kufanya kazi kwa usawa kana kwamba inaratibiwa na mtu mmoja.

Pacha Abby na Brittany wamekuwa mfano wa kuvutia ulimwenguni, wakithibitisha kuwa mapungufu ya kimaumbile si kikwazo cha kufanikisha ndoto. Kutoka kushiriki tamthilia ya televisheni, kufundisha, hadi kuingia kwenye ndoa, wameendelea kuvutia ulimwengu huku wakihifadhi faragha ya maisha yao ya mapenzi.
Kwa sasa, ulimwengu unasubiri kuona iwapo uvumi wa wao kuwa na mtoto utabadilika na kuwa ukweli, na hivyo kutimiza ahadi yao ya muda mrefu ya siku moja na wao kuwa mama.