Sowah apishana na Yanga Dar

MABADILIKO ya kalenda ya kuwania Ngao ya Jamii yameipa pigo Simba, ambayo sasa itakutana  na Yanga bila ya mshambuliaji mpya wa kikosi hicho, Jonathan Sowah aliyesajiliwa kutoka Singida BS.

Simba na Yanga zinatarajiwa kuzindua msimu mpya wa mashindano kwa mwaka 2025-2026 kwa kuvaana katika mechi ya Ngao ya Jamii iliyopangwa kupigwa Septemba 16 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.

Msimu huu mechi ya michuano hiyo haitashirikisha timu nne tofauti na ilivyokuwa kwa misimu miwili iliyopita ambapo, hesabu za Simba zilikuwa kumkosa mechi ya nusu fainali, kisha kama itatinga fainali basi imtumie, lakini mambo yamebadilika na sasa straika huyo Mghana anapishana na Yanga.

Ndio, huenda umepitiwa kidogo. Sowah alilimwa kadi nyekundu katika mechi ya fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) wakati akiitumikia Singida BS iliyopoteza mbele ya Yanga kwa mabao 2-0, mechi ikipigwa New Amaan Zanzibar, wafungaji wakiwa ni Dube Abuya na Clement Mzize. Sowah alipewa kadi hiyo dakika ya 86 iliyotokana na kupata kadi mbili za njano, kufuatia kukwaruzana na mabeki wa Yanga akiwemo Ibrahim Hamad ‘Bacca’ na mwamuzi Ahmed Arajiga kumtoa Mghana huyo, hivyo kumfanya atumikie adhabu ya kukosa mechi moja ya kimashindano.

Hivyo kutokana na mabadiliko ya kalenda hiyo ya mechi ya Ngao ya Jamii imezifuta mechi mbili za nusu fainali za michuano hiyo, ambapo kama zingekuwa basi ingewaokoa Wekundu kwa Sowah.

Mabadiliko hayo yameifanya mechi ya Ngao ya Jamii kubaki moja ambapo Yanga aliye mtetezi wa taji na anayemiliki ubingwa wa Ligi Kuu na Kombe la FA atacheza na Simba iliyomaliza nafasi ya pili msimu uliopita wa Ligi Kuu. Kama kungekuwa na nusu fainali, Simba ingevaana na Singida BS iliyomaliza ya nne, huku Yanga ingevaana na Azam FC iliyoshika nafasi ya tatu katika Ligi Kuu.

Kutokana na hali hiyo ni wazi, rasmi Sowah ataikosa mechi hiyo ya Ngao, kutokana na adhabu hiyo ambapo itakuwa ni pigo kwa Simba ambayo imemsajili kuongeza nguvu kwenye safu yao ya ushambuliaji.

Kukosekana kwa Sowah, kutaifanya Simba kusalia na washambuliaji Steven Mukwala, Seleman Mwalimu ambaye anasubiri kutambulishwa, kwani inadaiwa Leonel Ateba alikuwa katika mipango ya kuuzwa kama ilivyo kwa Valentino Mashaka anayedaiwa anajiandaa kutua JKT Tanzania.

Katika msimu uliopita Simba ilipoteza kwa bao 1-0 mbele ya Yanga mechi ya nusu fainali, kisha kwenda kushika nafasi ya tatu kwa kuifunga Coastal Union pia kwa baoa 1-0, wakati Yanga ilibeba tajio kwa kuikandika Azam FC kwa mabao 4-1. Azam ilifika fainali ya kuifunga Coastal mjini Unguja.

Mkurugenzi wa Mashindano wa TFF Salum Madadi, amelithibitishia Mwanaspoti kuwa, adhabu ambazo zilitolewa katika mechi za mwisho, zitaanza kutumika kuanzia mechi ya Ngao ya Jamii.

“Kama ambavyo kanuni zinaelekeza, kama kulikuwa na adhabu kwenye mechi za mwisho kwenye kufunga msimu uliopita, basi mchezaji au timu husika zitaanza kutumika kuanzia mchezo wa Ngao ya Jamii,” alisema Madadi.