Tarime. Halmashauri ya Wilaya ya Musoma Vijijini mkoani Mara imetenga zaidi ya Sh280 milioni kwa ajili ya kutekeleza miradi ya nishati safi ya kupikia katika shule 22 za msingi na sekondari zilizopo ndani ya halmashauri hiyo.
Bajeti hiyo inayotokana na mapato ya ndani, ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan alilolitoa kwa taasisi za umma zinazotoa huduma ya chakula kwa watu zaidi ya 100, kuanza kupika kwa kutumia nishati safi ya kupikia badala ya kuni na mkaa.
Akitoa taarifa kwa kiongozi wa mbio za Mwenge leo Agosti 21, 2025 kwenye uzinduzi wa mradi wa nishati safi ya kupikia katika Shule ya Sekondari Julius Kambarage, Ofisa Mazingira wa halmashauri hiyo, Annastazia Chami amesema fedha hizo zinatarajiwa kusimika mitambo ya gesi katika shule hizo kwa mwaka 2025/26.
“Hadi sasa tayari shule 16 za msingi na sekondari katika halmashauri yetu zimekamilisha miradi hii na kuanza kutumia gesi katika mapishi yao, tunatarajia shule nyingine sita za msingi na sekondari kukamilisha miradi hii hadi ifikapo mwaka 2026,” amesema.
Chami amesema lengo la halmashauri hiyo ni kuhakikisha shule zote 188 za umma za sekondari na msingi zilizopo katika halmashauri hiyo zinatumia nishati safi ya kupikia ifikapo 2029/30.
Akizungumzia mradi huo, Kiongozi wa mbio za Mwenge kitaifa, Ismail Ussi amesema umefika wakati sasa jamii nzima iachane na matumizi ya kuni na mkaa na kuhamia kwenye nishati safi ya kupikia.

Kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa, Ismail Ussi akizungumza wakati wa mbio za mwenge katika halmashauri ya wilaya ya Tarime vijijini. Picha na Beldina Nyakeke
Amesema lengo la Rais Samia Suluhu Hassan katika kuhimiza matumizi ya nishati safi pamoja na mambo mengine ni kutaka kulinda afya za wananchi kutokana na madhara ya kiafya kwenye matumizi ya kuni na mkaa sambamba na uharibifu wa mazingira.
“Mkurugenzi na timu yako hongereni sana lakini sasa niwaombe tuhakikishe taasisi zote zilizopo chini yako zinahamia kwenye nishati safi na salama, hii ni mbali na faida za kiafya lakini pia itaendelea kumjengea Rais wetu heshima ambayo amejipatia ndani ya nchi na kwenye bara la Afrika kwa kuwa kinara wa uhamasishaji juu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia,” amesema.
Wakati huohuo, mgodi wa dhahabu wa Barrick North Mara, kupitia mpango wa uwajibikaji kwa jamii (CSR), umetumia zaidi ya Sh2.7 bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi miwili ya afya na maji katika vijiji vya Mangucha na Nyamongo wilayani Tarime.
Miradi hiyo ni miongoni mwa iliyowekewa mawe ya msingi na mbio za mwenge huku wananchi wakishukuru kwa utekelezaji wake, kwani itasaidia kutatua changamoto walizokuwa nazo kwa sekta hizo za afya na maji.
Mradi wa ujenzi wa zahanati katika kijiji cha Mangucha unatarajiwa kunufaisha wakazi wapatao 4,460 umegharimu zaidi ya Sh164 milioni ulianza kutekelezwa Juni mwaka huu na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu.
Mradi wa maji unatekelezwa katika eneo la Nyamongo kwa gharama ya zaidi ya Sh2.6 bilioni ambapo unatarajiwa kunufaisha wakazi zaidi ya 46,000 wanaozunguka mgodi huo.
Akizungumza baada ya kuweka mawe ya msingi katika miradi hiyo, Ussi amesema utekelezaji wa miradi hiyo unatokana na uwepo wa sera nzuri za uwekezaji nchini.
Hivyo amewataka wananchi kuhakikisha wanashiriki kwenye uchaguzi mkuu kwa amani na utulivu ili kutoa fursa kwa wawekezaji wengi zaidi kuwekeza.
“Ili tupate maendeleo yetu na nchi ni lazima kuwe na amani na utulivu hivyo niwahimize wote wenye sifa za kupiga kura na kushiriki kwenye uchaguzi huu tuhakikishe tunashiriki kikamilifu.
“Kwa yule ambaye alikuwa amepanga kwenda kwenye shughuli nyingine Oktoba 29, hebu weka ratiba yako vizuri siku hiyo nenda kapige kura kwanza ndipo uendelee na ratiba nyingine,” amesema Ussi.
Amesema mradi wa maji ukikamilika utasaidia kufikia lengo la Serikali la upatikanaji wa maji kwa asilimia 85 kwa maeneo ya vijijini ifikapo Desemba 2025.