Iringa. Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umeendelea kuendesha ziara za mafunzo kwa wahifadhi, kwa lengo la kujengea ujuzi na uelewa wa kushughulikia mashamba ya miti na kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao.
Wahifadhi 15 kutoka Shamba la Miti Buhigwe – Makere walitembelea Shamba la Miti Sao Hill, wilayani Mufindi, Agosti 20, 2025, kujionea jinsi shughuli za kila siku zinavyofanyika shambani hapo. Ziara iliongozwa na Mhifadhi Mkuu Deogratius Kavishe.
“Tumefika hapa kuona jinsi kazi zinavyofanyika ili tukirudi shambani kwetu tuwe na elimu mpya ya uendelezaji wa shamba,” alisema Kavishe.
“Tumepata mafunzo ya ufugaji wa nyuki, utatiki wa mbegu, upandaji wa miche, kupogolea, usafishaji wa mashamba na upunguzaji wa miti dhaifu kupata mazao bora.”
Wahifadhi hao pia walitembelea kiwanda cha uchakataji wa mazao ya nyuki, duka la kuuza mazao, bustani ya miche, na maeneo ya uvunaji wa utomvu wa miti. Ziara ilihitimishwa kwa kutembelea maeneo ya vivutio vya utalii vilivyopo shambani, wakiangalia mandhari ya kupendeza inayojulikana kama “Bahari ya Miti.”
Wahifadhi hao wametoa pongezi zao kwa Kamishna wa Uhifadhi TFS, Prof. Dos Santos Silayo, kwa kuwawezesha kupata uelewa zaidi wa mashamba ya miti na kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao.
TFS inasema ziara kama hizi ni njia muhimu ya kujenga uwezo wa wahifadhi na kuboresha utendaji wao wa kila siku, jambo linalochangia matokeo chanya katika utunzaji wa misitu na uchumi wa mazao ya misitu.