Moshi. Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour Party (TLP), Richard Lyimo amesema chama hicho hakitakufa licha ya kifo cha aliyekuwa kiongozi wake, marehemu Augustino Mrema, badala yake kitaendelea kuimarika kisiasa.
Akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika leo Alhamisi Agosti 21, 2025, katika eneo la Njiapanda ya Himo wilayani Moshi, mkoani Kilimanjaro, Lyimo amesema TLP bado kina viongozi imara watakaolinda urithi wa Mrema na kuendeleza mapambano ya kisiasa.
“Wapo waliodhani baada ya Mrema kutangulia mbele ya haki TLP itakufa. Lakini chama kina viongozi wengi. Mimi niliyekuwa Katibu Mkuu, sasa ndiye Mwenyekiti. Safari inaendelea,” amesema Lyimo.
Lyimo alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa TLP Februari 2, mwaka huu, baada ya Mrema kufariki dunia Agosti 21, 2022.

Wanachama wa Chama cha TLP wakishiriki maandamano ya kumkaribisha Mwenyekiti wao, Richard Lyimo, aliyewasili kuzungumza nao katika mkutano uliofanyika leo, Agosti 21, 2025, eneo la Njia Panda, Himo, Moshi, Kilimanjaro. Picha na Yese Tunuka
Amesema chama kimeendelea kuimarika na kipo katika maandalizi ya kuongoza katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Jumatano Oktoba 29, 2025 na zingine zitakazokuja.
Katika mkutano huo, Lyimo ametangaza rasmi kuwa kesho atachukua fomu ya kugombea ubunge wa Jimbo la Vunjo kupitia TLP, akibainisha kuwa uamuzi huo ni matokeo ya ushauri kutoka kwa wazee wa jimbo hilo na uamuzi wa chama chake.
“Kwa kuwa chama kimeshanipitisha na wazee wa Vunjo wamenishauri nigombee, kesho nitachukua fomu Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kuomba ridhaa ya kuongoza wananchi kupitia nafasi ya ubunge,” amesema Lyimo.
Kauli za viongozi na wanachama
Katibu Mwenezi wa TLP Taifa, Elinihaki Mbwambo amesema mkutano huo ulikuwa sehemu ya ziara ya Mwenyekiti wa Taifa kwa ajili ya kuhamasisha na kuamsha ari ya wanachama wa chama hicho.
“Unajua chama kilikuwa kimeshuka, lakini sasa kimeamua kuamka. Pia ametangaza nia ya kugombea ubunge wa Vunjo na kesho tutampeleka ofisi za Halmashauri ya Moshi Vijijini kuchukua fomu,” amesema Mbwambo.

Baadhi ya wanachama waliohudhuria mkutano huo wameonyesha matumaini mapya kwa uongozi wa Lyimo.
Diana Maleko amesema: “Tunaamini Lyimo ataendeleza misimamo ya Mrema na kuleta uhai mpya kwa chama. Hatutaki TLP ionekane imekufa.”
Kwa upande wake, Thomas Kileo amesema“Ni wakati wa kuunganisha nguvu. Kifo cha Mrema kilileta pengo, lakini Lyimo anaonekana tayari kuendeleza mapambano ya kisiasa.”