Moshi. Serikali imesema uchunguzi wa awali uliofanywa kuhusu Hospitali ya Rufaa ya mkoa, Mawenzi kutoa huduma isiyoridhisha kwa wagonjwa umebaini changamoto kadhaa ikiwemo baadhi ya watumishi kutoroka kazini saa wa kazi na kusababisha ucheleweshwaji wa utoaji wa huduma.
Hatua hiyo imekuja baada ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, kueleza kusikitishwa na namna hospitali hiyo ilivyomcheleweshea huduma kwa saa tatu wakati alipompeleka mwanaye kupata huduma hospitalini hapo.
Agosti 12, 2025, mkuu huyo wa mkoa akiwa kwenye kikao cha tathmini ya hali ya lishe ya mwaka 2024/2025 cha mkoa huo, alieleza kuwa alifika hospitalini hapo akiwa amevalia kanzu na kofia kama mwananchi wa kawaida, ambapo wahudumu walimhudumia kwa kiwango kisichoridhisha bila kumtambua.
Akizungumza na Mwananchi leo Alhamisi Agosti 21, 2025, Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, Kiseo Nzowa, amesema ufuatiliaji wa tukio hilo tayari umefanyika na uchunguzi umebaini kuwepo kwa uzembe katika uwajibikaji.
“Moja ya tatizo ambalo limeonekana pale ni uwajibikaji kwa baadhi ya watumishi unakuwa sio ule unaotakiwa. Baadhi ya watumishi wanakuja kazini wanajiorodhesha kama wamefika halafu baada ya nusu saa anatoka na mbaya zaidi anaenda kufanya kazi kwenye taasisi nyingine ikiwemo hospitali za nje” amesema Nzowa.
Ameongeza kuwa, “Yaani wewe umeajiriwa Hospitali ya Mawenzi na saa zako za kazi ni mpaka saa 9:30 alasiri. Sasa baadhi yao wanatoka wanakwenda kufanya kazi nje kama vibarua hii kitu haitakiwi ni kinyume cha taratibu za utumishi wa umma.”
Aidha amesema changamoto nyingine iliyobainika ni baadhi ya wakuu wa idara kushindwa kuwasimamia ipasavyo watumishi walioko chini yao, hali inayosababisha baadhi yao kuingia na kuondoka kazini muda wanaotaka.
“Changamoto nyingine imeonekana baadhi ya wakuu wa idara hawana usimamizi madhubuti wa watu wao wanaowasimamia. Kama kiongozi inapaswa waliopo chini yako uwasimamie kikamilifu lakini wengine hawawajibiki kuwasimamia walioko chini yao kama knaavyopasa na hii ndiyo inasababisha baadhi kuingia kazini na kutoka muda wanaotaka.”
Ameongeza kiwa, “Pia kuna upotevu wa mapato katika baadhi ya idara na upotevu huu unatokana na baadhi ya watumishi wasio waaminifu ambao sasa wanachukua wagonjwa na kuwatibu kinyemela bila malipo halisi kuingia kwenye mfumo wa malipo ya hospitali sasa hili nalo ni tatizo linguine.”
Amesema, “Kwa hiyo niseme tatizo la kutokuwa waadilifu na utoro kwa visingizio wengine wanatengeneza mazingira ya uongo ya kuomba ruhusa, wakati mwingine wanasema wanaumwa lakini ukifuatilia yuko mtaani sasa hili tunataka likomeshwe.”
Amesema malalamiko siyo ya mkuu wa mkoa pekee bali pia wapo baadhi ya wananchi ambao wamewasilisha malalamiko ya kupata huduma zisizoridhisha katika hospitali hiyo.
Wapo wananchi ambao wamelalamika huduma katika hospitali yetu ya Mawenzi, hawaridhishwi na hawafurahishwi na huduma zinazotolewa. Ni jambo la kusikitisha sana kwamba baadi ya watumishi hawajitumi na hawatimizi wajibu wao ni lazima wajirekebishe kabla mkono wa serikali haujawafikia.”
Nzowa amebainisha kuwa hospitali hiyo imenufaika kwa kiasi kikubwa na uwekezaji wa vifaa tiba na watumishi kutoka serikakini hivyo hakuna sababu ya kuwepo malalamiko ya huduma duni.
“Ufuatiliaji unaendelea na wizara ya afya inalijua hili na zipo hatua zitachukuliwa muda si mrefu. Niendelee kutoa wito kwa watumishi wafanye kazi kwa mujibu wa taratibu kwani hatua zitachukuliwa kwa wale watakaobainika kwenda kinyume cha utendaji na viapo vyao vya utumishi vya kuwatumikia wananchi.”