Mbeya. “Elimu ije kwa wananchi,” ni kauli ya baadhi ya wakazi wa mitaa mbalimbali Wilaya ya Mbeya Vijijini huku wakielezea kikwazo cha kutekeleza mkakati wa Serikali kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.
Shabaha ya mkakati huo ni kuandaa programu za elimu na uhamasishaji kuhusu nishati safi ya kupikia.
Wakizungumza na Mwananchi baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Utengule, wanasema pamoja na juhudi zinazofanywa na Serikali katika matumizi ya nishati safi, bado elimu haijawafikia.
Ezekiel Mwamwaja anasema taarifa nyingi za matumizi ya nishati safi ya kupikia wanaziona na kuzisikia kwenye vyombo vya habari na si kiongozi yeyote kufika maeneo ya vijijini, hivyo wanadai kukosa elimu ya kina.
“Nadhani wanazungumzia kwenye vikao kisha wanatuma taarifa kwenye vyombo vya habari, kampeni kama hizi zinapaswa kufanyika kwa uwazi ili wananchi waweze kushauri na kupendekeza.
“Yapo mambo mengi tunahitaji kufahamu, mathalani nishati hii inahitaji gharama na vifaa kama majiko, gharama na mazingira rafiki, sisi tuishio vijijini inatupa wakati mgumu kufikia malengo hayo,” anasema Mwamwaja akiashiria wanahitaji kufahamu gharama wanawezaje kuzimudu.
Rehema Mwampashi, mkazi wa eneo hilo anasema jukumu hilo lilipaswa kukabidhiwa kwa viongozi wa Serikali za mitaa wanaoishi na wananchi ngazi za chini ili kila kaya iweze kuondokana na matumizi ya nishati chafu ya kupikia.
“Labda kuna taasisi au makundi maalumu yaliyolengwa, ila kama ni wananchi wote, naona bado kuna upungufu kwa kuwa familia nyingi zinatumia mkaa wa kuni na kuni zenyewe, viongozi wa mitaa ndio wangepewa jukumu kwa ngazi za chini,” anasema Rehema.

Mwandishi alifika katika Kiwanda cha Mbeya Kijana Wajibika (Mbekiwa) kilichopo Mbeya Vijijini na kushuhudia shughuli za uzalishaji wa mkaa mbadala, huku watalaamu wakielezea mafanikio, changamoto na ushauri ili kufikia malengo.
Mwenyekiti wa kikundi hicho, Sylivester Chawe anasema tangu kuanzishwa kwa kiwanda hicho, wamefanikiwa kupunguza uharibifu wa mazingira, japokuwa bado kuna changamoto kwenye jamii.
Chawe anasema mwitikio wa wananchi wa kuunga mkono juhudi hizo, si mzuri sana kutokana na hali ya mazingira kiuchumi na elimu kutokuwa rafiki kwa watumiaji huku akiomba Serikali kuingiza mkono kwa wazalishaji.
Anasema ili kufikia malengo, Serikali ifanye uamuzi wa kuwapa ruzuku wazalishaji kwa ajili ya kurahisisha bei sokoni na kuweka msisitizo kwa jamii katika kutotumia nishati chafu ya kupikia.
“Tatizo kubwa ni bei ya mkaa wetu ikilinganishwa na mkaa wa kuni, huko mtaani, Serikali inaweza kuamua kuweka ruzuku katika mkaa huu mbadala ili kuwarahisishia wananchi kuendana na sera,”anasema Chawe.
“Mkaa huu unahitaji majiko banifu ambayo ni tofauti na ile ya mkaa wa kuni, sasa wananchi hawajui kuhusu miundombinu hii, elimu pia bado haijawafikia moja kwa moja, kujua madhara na faida ya nishati hizi.”
Anasema baada ya mkaa kuzalishwa na kukaushwa, unawekwa katika ujazo tofauti kuanzia kilo moja mpaka kilo 10 huku kilo moja kuuzwa kwa bei ya Sh1,000 gharama yenye uwezo wa kupikia kwa siku nzima kwa familia ya watu watatu.
Chawe anasema kwa sasa kiwanda hicho kinaweza kuzalisha tani tatu kwa wiki, japokuwa malengo ni kuzalisha kiwango hicho kwa siku baada ya kupata sapoti ya kutosha kutoka serikalini.
Anasema matarajio yao ni kuzalisha pia majiko banifu ili Mtanzania yeyote anayefika kiwandani hapo kuchukua mzigo apate elimu na kwamba, hadi sasa wamefanikiwa kushawishi baadhi ya taasisi za Serikali na vituo binafsi kutumia nishati safi ya kupikia.
“Kuwepo katazo na msisitizo mkali kwenye matumizi ya nishati chafu, Mbekiwa tayari tumeshawishi vituo kadhaa ikiwamo kituo cha kulelea yatima wilayani hapa, hivyo taasisi zote za Serikali na binafsi zihimizwe iwe ni lazima,” anasema Chawe.
Anasema kwa sasa wanazalisha mkaa mbadala kwa kutumia mabaki ya mimea na takataka nyingine ngumu kwa lengo la kutunza mazingira na afya kwa wananchi.
Mtafiti na mbunifu wa mkaa mbadala, Abel Kibona anasema mkaa mbadala hauna harufu mbaya na ni rafiki kwa kupikia, kutunza mazingira na kuondokana na ukataji miti.
“Tatizo la kutokuwapo mwitikio ni kutokana na miundombinu ya vifaa, Serikali iwekeze kwa kutoa ruzuku kwa vikundi ili kuondoa gharama kwa wananchi.
“Serikali iwaunganishe wabunifu na kuwawekea mazingira ya ndani na nje kuongeza uzoefu na kujengewa uwezo ili kufikia malengo ya Tanzania katika kutekeleza mpango huu,” anasema Kibona.
Mkuu wa shule ya sekondari ya kutwa ya Mbeya, Francis Mwakihaba anasema muda wowote kuanzia wanatarajia kuanza matumizi ya nishati safi kwa kuwa miundombinu imewekwa tayari.
Pamoja na matumizi hayo, pia wanafikiria kutumia nishati jadidifu ikiwa ni baiogesi itakayoambatana na elimu kwa wanafunzi.
“Wakati tukitumia mkaa mbadala, lakini tunafikiria kutumia zile gesi na tunatarajia kuwatumia wanafunzi wetu kuliko kuwategemea wazabuni, tumeshaanza kupata elimu kutoka kwa watalaamu kwa kutumia karatasi,” anasema Mwakihaba.
Anasema matumizi ya nishati hiyo yatasaidia uhifadhi mazingira, afya na kupunguza gharama kubwa ikilinganishwa na matumizi ya kuni, akieleza kuwa shule hiyo imejipanga kutoa elimu kwa walezi na wazazi.
“Kila mwanafunzi ataelimishwa faida za matumizi ya nishati safi ili kuwa mabalozi kwenye familia zao, lakini wazazi na walezi nao watakuwa wakielimishwa ili nishati hii ianzie nyumbani,” anasema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Justice Kijazi anasema matumizi ya nishati safi ni njia sahihi katika utunzaji mazingira na kuepuka athari za kiafya na ikolojia kwa wananchi.
Pia, anasema katika kufanikisha hilo, upo mkakati unaoendelea katika halmashauri hiyo kwa kuwaunga mkono wananchi na makundi yanayojishughulisha na utunzaji mazingira.
“Kupitia halmashauri tunatoa elimu na ile mikopo ya asilimia 10 tunayafikia makundi yale yanayotengeneza mkaa mbadala na majiko banifu, tunashauri wananchi kutumia zaidi nishati hii kwa maendeleo,” anasema Kijazi.
Habari hii imedhaminiwa na Bill & Melinda Gates Foundation
Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917