Mwanza. Watuhumiwa watatu wa mauaji ya Nestory Marcel yaliyotekelezwa Juni 23, 2025, katika eneo la Buganda, Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza, wamefikishwa mahakamani.
Watuhumiwa hao ni Jacob Odhiambo (36) ambaye ni mfanyabiashara na mkazi wa Buswelu, Abdul Dinisha (29), mfanyabiashara kutoka Nyamhongolo na Erick Olang (37), mfanyabiashara na mkazi wa Igoma.
Akisoma hati ya mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi, Stellah Kiama, Wakili wa Serikali, Mwanahawa Changale amesema watatu hao wanadaiwa kumuua Marcel Juni 23, 2025, katika eneo la Buganda, Wilaya ya Ilemela.

Tukio hilo wanalodaiwa kulifanya kwa pamoja ni kinyume na vifungu vya 196 na 197 vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, marejeo ya mwaka 2023.
Hata hivyo, Hakimu Kiama amesema washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote kwani Mahakama ya wilaya haina mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji.
“Kwa msingi huo, Mahakama hii haina uwezo wa kusikiliza shtaka linalowakabili. Utaratibu utakapo kamilika, kesi ya msingi itapelekwa Mahakama Kuu kwa hatua zaidi,” amesema Kiama.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Septemba 4, 2025 kwa ajili ya kutajwa tena.