Yanga, Simba zachomoa tena Kagame Cup 2025

WAKATI Shirikisho la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) likitangaza timu 12 zitashiriki mashindano ya Kombe la Kagame 2025 zikiwemo Yanga na Simba, wakongwe hao wa soka la Tanzania wameamua kujiweka pembeni huku sababu za kufanya hivyo zikitajwa.

Uamuzi wa timu hizo kujiweka pembeni umetajwa ni kutokana na ratiba kuwabana kufuatia uwepo wa matamasha yao ya kila mwaka ambayo yamepangwa kufanyika wakati mashindano hayo yakiendelea.

Sambamba na hilo, uwepo wa mchezo wa Ngao ya Jamii utakaozikutanisha timu hizo uliopangwa kufanyika Septemba 16, mwaka huu, ikiwa ni siku moja baada ya fainali ya Kombe la Kagame, nayo ni sababu nyingine.

Kwa mujibu wa CECAFA, michuano ya Kombe la Kagame inatarajiwa kufanyika Dar es Salaam kuanzia Septemba 2 hadi 15 mwaka huu ikishirikisha timu 12 kama ilivyokuwa mwaka jana.

Taarifa ilizozipata Mwanaspoti kutoka ndani ya Yanga zinabainisha kwamba, uamuzi wa kutoshiriki mashindano hayo umekuja ili kutoa muda mwingi wa benchi la ufundi kuiandaa timu na pia ratiba hiyo imeingiliana na Tamasha la Wiki ya Mwananchi linalotarajiwa kufanyika Septemba 6 mwaka huu ikiwa ni msimu wa saba tangu kuanza kwake mwaka 2019.

“Yanga haitashiriki michuano ya Kagame mwaka huu kwa sababu tuna ratiba ngumu iliyo mbele yetu,” kilisema chanzo kutoka Yanga na kuongeza.

“Tangu tuanze maandalizi ya msimu mpya kikosi hakina wachezaji wote kwani wengine wanaitumikia Taifa Stars inayoshiriki michuano ya Chan, lakini pia tuna tamasha letu la Wiki ya Mwananchi tunalolifanya kila mwaka, hivyo haitawezekana tushiriki mashindano ambayo katikati yake tuwe na tamasha letu.”

Kwa upande wa Simba, taarifa za ndani zinasema haitashiriki michuano hiyo huku ikiwa tayari imetangaza Septemba 10 mwaka huu itakuwa na Tamasha la Simba Day ambalo linakwenda kufanyika kwa msimu wa 17 tangu lilipoanza mwaka 2009.

Hivi sasa Simba ipo Misri ikiwa imepiga kambi ya maandalizi ya msimu wa 2025-2026 ambapo ilifika huko tangu Julai 30 mwaka huu na inatarajiwa kurejea nchini mwanzoni mwa Septemba.

Yanga ipo jijini Dar es Salaam na jana jioni ilitarajiwa kuingia rasmi kambini Avic Town huko Kigamboni kuendelea na maandalizi yao yaliyoanza tangu mwishoni wa Julai mwaka huu.

Hii haitakuwa mara ya kwanza kwa timu hizo kutoshiriki mashindano hayo kwani mwaka jana zilifanya hivyo pia huku ikielezwa Yanga ilichukua uamuzi huo kutokana na wachezaji wake wengi kuwa likizo.

Agosti 5 mwaka huu, Mkurugenzi Mtendaji wa CECAFA, Auka Gecheo, alitangaza uwepo wa mashindano hayo ya Kagame akisema: “Tunayo furaha kutangaza kwamba mashindano haya yatafanyika kuanzia Septemba 2 hadi 15 jijini Dar es Salaam, Tanzania.”

Gecheo alisisitiza kwamba, jumla ya timu 12 zitashiriki, ambapo wenyeji Tanzania watatoa timu mbili na pia kutakuwa na timu moja mualikwa kutoka ukanda mwingine.

“Tunatarajia kuona mashindano yenye ushindani mkubwa zaidi kwani timu nyingi zitayatumia kama maandalizi ya mashindano ya CAF msimu wa 2025/2026,” aliongeza Gecheo.

Mwaka jana, timu ya Red Arrows kutoka Zambia ilitwaa Kombe la Kagame baada ya kuifunga APR FC ya Rwanda kwenye mchezo wa fainali uliochezwa Uwanja wa KMC uliopo Mwenge jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa CECAFA, timu wanazotarajia kushiriki mashindano hayo ni Vipers SC (Uganda), El Merriekh SC Bentiu (Sudan Kusini), Mlandege SC (Zanzibar), Al Hilal (Sudan), Kenya Police FC (Kenya), Ethiopia Insurance (Ethiopia), Mogadishu City Club (Somalia), APR FC (Rwanda), Aigle Noir FC (Burundi), Yanga (Tanzania), Simba SC (Tanzania) na ASAS Djibouti Telecom (Djibouti).

Michuano hiyo mwaka jana ilifanyika pia jijini Dar es Salaam kwenye viwanja vya Azam Complex na KMC huku Tanzania Bara ikiwakilishwa na Singida Black Stars na Coastal Union wakati JKU ikitokea Zanzibar.

Timu 12 zilishiriki mashindano hayo ambapo bingwa alikuwa Red Arrows ya Zambia, huku APR ya Rwanda ikikamata nafasi ya pili, Al Hilal ya Sudan ya tatu na Hay Al-Wadi SC nayo kutoka Sudan ikishika nafasi ya nne. Zingine zilizoshiriki michuano hiyo iliyoanza Julai 9 hadi 21 mwaka jana ni Al-Merreikh Bentiu (Sudan Kusini), AS Ali Sabieh (Djibouti), Coastal Union (Tanzania), Dekedaha (Somalia), Gor Mahia (Kenya), JKU (Zanzibar), Singida Black Stars (Tanzania) na SC Villa (Uganda).