Bodaboda, bajaji watajwa vyanzo vya ajali Geita

Geita. Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Geita (GGML) kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, imezindua kampeni ya uhamasishaji kuhusu usalama barabarani, lengo kukabiliana na ajali za barabarani.

Kampeni hiyo inalenga hasa madereva wa bodaboda na bajaji, kufuatia takwimu zinazoonyesha kuwa vyombo hivyo vya usafiri vinaongoza kwa kusababisha ajali nyingi barabarani.

Akizungumza Agosti 22, 2025 wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo, Mkuu wa Polisi Wilaya ya Geita, Renatus Katembo amesema kundi kubwa la vijana linaendesha bodaboda na bajaji kwa ajili ya kipato, lakini mara nyingi hawazingatii sheria za usalama barabarani.

Bila kutaja takwimu za ajali zilizotokea wilayani humo, mkuu huyo wa polisi amesema waathirika wakuu wa ajali ni madereva wa bodaboda na bajaji na mara nyingi wamekuwa wakisimama maeneo yasiyoruhusiwa.

“Mara nyingi bajaji na bodaboda hamzingatii sheria za usalama barabarani, mnasimama ghafla sehemu iisiyo ruhusiwa, mnapakia abiria bila tahadhari na kuvuka sehemu zisizo rasmi na takwimu zinaonyesha wanaopata ajali ni nyie bajaji na bodaboda kwa kusababisha au kusababiishiwa na hii inasababisha madhara kwenu na vyombo vyenu, lakini madhara kwa abiria na watumiaji wengine wa barabara,” amesema Katembo.

Katembo amesema kazi hiyo inabeba kundi kubwa la vijana wanaojiitafutia kipato kwa njia ya halali na kuwataka watambue kuwa wao ni kiungo muhimu katika jamiii kwenye sekta ya usafirishaji na uzalishaji mali hivyo wanapaswa kuwa makini na kuzingatia usalama barabarani.

Katika hatua nyingine Katembo amewataka madereva bodaboda wanaotumiwa na vyama vya siasa  wakati huu wa kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu kutotumia vibaya barabara kwa kuzifunga bila kujali watumiaji wengine wa barabara.

Kwa upande wake, Mwakilishi  kutoka GGML, Elibariki Jambau aliyemwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, amesema kampeni hiyo imelenga kuwafikia madereva 932, wa bodaboda na bajaji ambapo kwa kuanza wameanza na 491.

“Kampeni hii inakwenda sambamba na kaulimbiu ‘Uendeshaji salama unaanza na wewe.’ Tunataka kila dereva aelewe kuwa kipimo cha ushindi si mwendo wa haraka, bali ni kufika salama na kurejea kwenye familia yako ukiwa salama,” amesema Jambau.

Amesema mbali na mafunzo ya siku tatu madereva watapewa pia ‘reflekta’ ili kuwasaidia nyakati za usiku, na shule 12 zitapatiwa elimu ya usalama barabarani.

Mwenyekiti wa madereva bajaji Wilaya ya Geita, Fredy Fidel ameishukuru GGML kwa mpango huo ambao utawasaidia kujua alama za barabarani na sheria ambazo kwa kuzijua zitawarahisishia upatikanaji wa leseni na vyeti kwa madereva.

“Vijana wengi hawana elimu ya udereva wala leseni wanaendesha kwa uzoefu, lakini mafunzo yanayotolewa yatasaidia kuwajengea uelewa na kuepusha ajali zisizo za lazima barabarani.

“Mafunzo haya yataokoa maisha, lakini pia tunahitaji vituo rasmi vya kupakia na kushusha abiria ili kupunguza vurugu na ajali,” amesema Kisoke.

Mwenyekiti wa Umoja wa madereva bajaji mkoani Geita amesema changamoto inayosababisha kusimama maeneo yasiyoruhusiwa inatokana na ukosefu wa vituo maalum vya kuegesha na kuiomba serikali kuweka maeneo ya maegesho ili kuweka mazingira rafiki kwao na abiria.

Takwimu zinaonyesha kati ya mwaka 2022 hadi 2024, jumla ya wananchi 1,113  wamepoteza maisha kutokana na ajali zinazosababishwa na bodaboda nchini.

Kwa mujibu wa takwimu hizo madereva pikipiki waliopata ajali na kufariki dunia ni 759, abiria ni 283 huku watembea kwa miguu waliopoteza maisha ni 71.

Kwa mujibu wa takwimu za Jeshi la Polisi, kati ya mwaka 2019 hadi 2023, ajali 10,174 ziliripotiwa nchini, sawa na wastani wa ajali 2,035 kwa mwaka.