ETDCO YANG’ARA TUZO YA MKANDARASI BORA MIUNDOMBINU YA UMEME 2025.

…………...

Kampuni ya ETDCO imeibuka mshindi wa kwanza katika kipengele cha Mkandarasi Bora wa Ujenzi wa Miundombinu ya Umeme (Outstanding Electrical Contractor of the Year – 2025) kwenye Tuzo za Dunia za Ujenzi (32nd World Construction Awards), zilizotolewa na Chamber of Construction and Infrastructure of Tanzania (CCIT) iliyofanyika  Agosti 21, 2025 katika Ukumbi wa Super Dome, Masaki, Dar es Salaam.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi katika hafla ya utoaji wa tuzo, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta, amesema kuwa Sekta ya ujenzi ni muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii, huku akitoa wito kwa washindi wa tuzo hizo kuzitumia kama chachu ya kuongeza bidii na ubunifu ili katika utekelezaji wa majukumu yao

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi wa ETDCO, Mhandisi Dismas Masawe, ameishukuru CCIT kwa kutambua mchango wa Kampuni hiyo katika Ujenzi wa miundombinu ya umeme, ambapo  meahidi kuwa ETDCO itaendelea kutoa huduma bora na zenye viwango ili kuchangia kwa ufanisi katika kukuza uchumi wa Taifa.

Mhandisi Masawe amebainisha kuwa tuzo hiyo ni motisha kwa Kampuni kuendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, huku akisisitiza kuwa Sekta ya ujenzi haiwezi kuendelea bila upatikanaji wa umeme wa uhakika.

Aidha, amefafanua kuwa katika kipindi hiki Cha Serikali ya Awamu ya Sita, ETDCO imefanikiwa kujenga miundombinu ya umeme ya kilovolti 132 kwa jumla ya kilomita 495. Miradi hiyo ni pamoja na kuunganisha huduma ya umeme kutoka Tabora hadi Katavi (km 383), Tabora hadi Urambo (km 115), pamoja na kupeleka umeme kwenye vitongoji 105 na vijiji 291 — hatua iliyochangia kwa kiasi kikubwa kuleta maendeleo kwa jamii.