Dar/Pwani. Imani potofu kuhusu ugonjwa wa mabusha bado zinatesa jamii za Pwani, ingawaje tiba ipo, lakini hofu na aibu zinazuia wengi kusaka matibabu, huku watu 778,415 wakitajwa kuwa hatarini.
Bagamoyo ni miongoni mwa wilaya tano, ambazo bado waathirika wa ugonjwa mabusha wamesalia, huku baadhi yao wakitafuta tiba za mitishamba na wengine kwa waganga wa kienyeji.
Tanzania ni moja ya nchi zilizoathiriwa zaidi na magonjwa yasiyopewa kipaumbele (NTDs) ikishika nafasi ya nane duniani na ya nne barani Afrika.
Mwaka 2023 zaidi ya watu milioni 36 barani Afrika walihitaji matibabu kwa angalau ugonjwa mmojawapo kati ya trakoma, minyoo, kichocho, mabusha na matende au usubi.
Shabanni Ramadhan (46) mkazi wa kijiji cha Rudiga Kata ya Talanda wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani, ni miongoni mwa waathirika wa magonjwa yasiyopewa kipaumbele.
Yeye aliishi na ugonjwa wa ngiri maji maarufu busha kwa takribani miaka 14 bila matibabu.
Aliishi kwa tiba za jadi, hata hivyo kitu cha kushtua zaidi ugonjwa wake huo ulichukuliwa kama mtu mwenye karama fulani (mwinyi), huku jamii inayomzunguka ikichukulia kama mtu mwenye thamani ya kipekee.
Ingawaje anasema hakufurahia hali hiyo na mara kadhaa alikuwa akitafuta tiba za jadi, Shabani aliishi na ugonjwa wa mabusha tangu mwaka 2010, ukiendelea kumnyima nguvu na hatimaye ukawa mzigo mkubwa kwake.
Akifanya kilimo kujikimu, alipambana kutunza familia yake huku akiwa na maumivu. Familia yake kubwa ilijaribu kuchangisha fedha ili kumpatia matibabu, lakini fedha zilizopatikana hazikutosha.
“Aprili 2024 nilipatiwa upasuaji na matibabu kwa msaada wa shirika la Sightsavers, na sasa nimerudi katika hali ya afya njema kabisa, naweza kulima mashamba yangu bila tabu. Nina matumaini ya kujenga nyumba ya kudumu kwa ajili ya watoto wangu na kuwekeza katika pikipiki,” anasema Shabani.
Kama ilivyo kwa Shabanni, ndivyo ilivyotokea kwa Tito Ibrahim, mkazi wa kijiji cha Fukayosi, Kata ya Fukayosi Wilaya ya Bagamoyo.
Tito anayesoma darasa la saba katika Shule ya Msingi Fukayosi, alizaliwa na ugonjwa huo kabla ya kupatiwa matibabu mwaka 2023 katika Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo, upasuaji uliowezekana kwa msaada wa End Fund na Sightsavers, wadau wanaotekeleza miradi ya tiba na kinga ya magonjwa yasiyopewa kipaumbele duniani.
Kabla ya upasuaji, Tito alikosa vipindi vya masomo shule mara kwa mara kutokana na hali yake, hasa wakati wa baridi na vipindi vya mvua.
Mlezi wake mkuu ni bibi yake, Rosemary Masanja maarufu Bibi Tito, anayesema hali ya mjukuu wake ilikuwa ikimuumiza kila wakati, na nyakati zote hakuweza kucheza vizuri, wala kuhudhuria masomo kama inavyotakiwa.
“Hata kama anacheza alikuwa anaacha anarudi nyumbani analalamika kwamba bibi tumbo linaniuma, anaenda ndani na kulala,” anasimulia na kuongeza:
“Shule alikuwa anaenda kila siku kipindi cha jua kali, kukiwa na mawingu hakuwa anaenda shule na kuna siku anaenda anarudi na nyakati nyingine haendi kabisa na mvua ikinyesha ilimuathiri zaidi.”
Anasema haikuwa rahisi kwani alihaha na tiba za jadi na kwa waganga ili mjukuu wake apone, hata hivyo hakufanikiwa mpaka alipopatiwa matibabu hospitalini.
“Wananiambia kuna dawa ya kienyeji kachimbe umpatie mtoto, lakini hazikisaidia. Tangu alipozaliwa korodani zake mbili moja ikawa inajaa maji tulipompeleka hospitali wakasema atafanyiwa upasuaji akifikisha umri wa miaka mitano.
“Baada ya miaka mitano hakufanyiwa upasuaji, hatukumpeleka sababu hatukuwa na kitu chochote, tulikuwa na changamoto za kifedha,”anaeleza bibi huyo.
Akielezea mabadiliko baada ya matibabu, anasema hivi sasa yupo vizuri anashiriki michezo na wenzake vizuri, mahudhurio ya shuleni hakosi na pia amenyanyuka kitaaluma.
“Baada ya kufanyiwa upasuaji anahudhuria shule kila siku, nyuma alikuwa nafasi ya 34 kwenda juu, baada ya upasuaji Tito sasa anashika nafasi ya 10 au ya nane darasani anapanda kila kukicha,” anasema Bibi Tito.
Alipozungumza na mwandishi, Titto anasema maisha yake kipindi cha nyuma hayakuwa na afadhali kwani alizoea kulala pindi anapohisi maumivu.
“Nilikuwa napata maumivu makali sana na kadri siku zinazozidi kwenda maumivu yale yalikuwa yanazidi. Ilifika hatua naumia sana nikiwa darasani na afadhali yangu siku zote ilikuwa kulala usingizi, nikilala maumivu yale yanaachia,” anaeleza.
Titto mwenye ndoto za kuwa mchezaji mpira nyota nchini, anasema alishindwa kushiriki vema katika michezo hasa mpira wa miguu anaohusudu zaidi kutokana na tatizo lake.
Mwalimu wa taaluma katika Shule ya Msingi Fukayosi anakosoma Titto, Neema Msuya anasema kabla ya matibabu, mahudhurio ya mtoto huyo shuleni hayakuwa mazuri kwani alikuwa anakaa nyumbani mara kwa mara na kukosa baadhi ya vipindi vya masomo.
“Lakini baada ya matibabu ameonyesha maendeleo makubwa katika mahudhurio, si mkosaji wa shule na amepanda kitaaluma tofauti na kipindi cha mwanzo, maendeleo yake yalikuwa mabovu,” anasema Mwalimu Msuya.
Akielezea ugonjwa wa Tito, Meneja udhibiti wa kutokomeza ugonjwa wa matende na mabusha, kutoka Mpango wa Taifa wa kudhibiti magonjwa yasiyopewa kipaumbele (NTDs) Wizara ya Afya, Dk Faraja Lyamuya, anasema hilo ni tatizo ambalo mtoto huyo alizaliwa nalo.
Anasema tatizo hilo lilitokana na mifumo ya mwili kuwa na sehemu au mishipa ambayo ilitakiwa iwe imeziba, lakini kwa bahati mbaya iliacha uwazi na kusababisha maji yakawa yanajaa na vitu ambavyo vilitakiwa kuwa kwenye tumbo vinashuka na kwenda suhemu za siri na ndiyo sababu huitwa ngiri kokoto.
Dk Lyamuya anasema mzazi anaweza kuona mtoto wake wa kiume anapata uvimbe sehemu zake za siri kwenye korodani moja inajaa maji, kuna wakati fulani akilia anaona sehemu za siri zinavimba na akiwa ametulia amelala zinarudi vizuri.
“Hii ni ishara kwamba ana ngiri maji au henia wanaitwa ngiri kokoto, Tito alizaliwa na vyote viwili ngiri maji na ngiri kokoto na ndiyo maana historia yake anasema akicheza alikuwa anasikia maumivu, hili ni tatizo watoto wachache wanazaliwa nalo,” anafafanua.
Kwa mujibu wa Dk Lyamuya, mtoto anaweza kukua nalo mpaka umri wa miaka mitano ndipo hushauriwa kufanyiwa upasuaji, hata hivyo humletea karaha.
“Madhara yake ni kwamba anapopata busha na henia huendelea kukua kadri muda unavyozidi kwenda. Kwa Tanzania tatizo hili lipo ila hakuna idadi kamili ya watoto wangapi wanazaliwa na tatizo hili la kimaumbile,” anasema.
Akizungumzia jitihada za Serikali katika kutokomeza ugonjwa huo, anasema vituo vingi vya afya vimekuwa vikifanya upasuaji wa henia na wengi hufanikiwa mapema wakubwa kwa wadogo.
Anasema Wizara ya Afya kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wanaendelea kuelimisha jamii, ingawaje bado kuna jamii ina imani potofu kwamba busha ni ufahari au umwinyi.
“Busha linatibika, madhara ya kuendelea kukaa na busha ni makubwa na mtu mwenye busha hapati maumivu ndiyo maana wameweza wengine kukaa nayo mpaka yanakuwa makubwa, lakini linapokuwa kubwa sana mtu anapata madhara ya kisaikolojia anapotembea watu wanamtania, wanamcheka, anakosa uhuru.
“Anashindwa kujichanganya na watu inavyostahili anaanza kujitenga, anashindwa kufanya shughuli zake kama kawaida sababu ya uzito hivyo hashiriki katika shughuli za kijamii na uchumi wake binafsi, huku wengine wakiachana au kutengana na wenza wao,” anaeleza.
Meneja wa Mpango wa Taifa wa kudhibiti magonjwa yasiyopewa kipaumbele (NTDs) Wizara ya Afya, Dk Clarer Mwansasu anasema mpaka kufikia mwaka 2024 zaidi ya wagonjwa 19,774 walipatiwa matibabu na jumla ya watu 12,660 walifanyiwa upasuaji kwa kipindi cha mwaka 2009/2024.
Amesema Tanzania ina magonjwa matano yanayolengwa kwa tiba kinga ikiwemo kichocho, minyoo ya matumbo, mabusha, usubi na trakoma ambayo yanaelekea kutokomezwa.
Anasema mafanikio haya yamechangiwa na mbinu shirikishi inayojumuisha utoaji wa dawa kinga kwa wingi, uhamasishaji wa jamii, upatikanaji bora wa huduma za afya, uimarishaji wa ufuatiliaji na utafiti.
“Mafanikio haya yametokana na uratibu thabiti kati ya jamii, Wizara ya Afya na wadau wa maendeleo, wakiwemo Sightsavers, The END Fund na wengineo. Pia tunaingiza fedha za NTDs katika mipango ya afya ya halmashauri na bajeti za kitaifa, sambamba na kuchunguza mbinu bunifu za ufadhili,’’ anasema.