KIKOSI cha Yanga kinaendelea kujifua jijini Dar es Salaam, huku kambi ikipokea ujio wa beki mpya kutoka Ghana, ambaye amepewa mkataba wa mwaka mmoja na tayari ameanza kufanya mambo chini ya kocha Romain Folz.
Yanga inajiandaa na mechi za msimu mpya wa 2025-26 ikiwania kutetea mataji matatu kwa mpigo, Ngao ya Jamii, Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho (FA) mbali na Kombe la Muungano na pia inajipanga kuboresha rekodi katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakayoanza rasmi mwezi ujao.
Ikiwa katika maandalizi hayo, hususani mechi ya Ngao ya Jamii ya kuzindua msimu itakayopigwa siku chache baada ya kutambulisha kikosi kipya katika tamasha la Wiki ya Mwananchi inayodaiwa itakuwa Septemba 12, Yanga imeshusha beki mpya aliyekuwa akikipiga Singida Black Stars, Frank Assinki.
Beki huyo tayari ameshajiunga kambini jana Alhamisi akiungana na wenzake mazoezini na mchana akatambulishwa rasmi, huku chanzo cha kuaminika kikilipenyezea Mwanaspoti kwamba jamaa amepewa mkataba wa mwaka mmoja wenye kipengele cha kumuongezea mwingine endapo akifika katika malengo ya klabu hiyo. Awali ilielezwa ametua kwa mkopo wa miezi sita toka SBS.
Kusajiliwa kwa Assinki kunakwenda kumuondoa katika mfumo wa usajili, beki wa kulia wa timu hiyo aliye majeruhi, Kouassi Yao ambaye msimu uliyopita alitumika mechi saba akicheza kwa dakika 538.
“Assinki alifika kambini jana (juzi) usiku ila mazoezi ameanza kuyafanya leo (jana) na wenzake, hadi Yanga tunamsajili tumemuona ni beki anayeweza akaongeza nguvu katika eneo hilo, ila kiwango chake ndicho kitakachoamua kumuongezea mkataba mwingine,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;
“Ingawa Yanga bado tuna imani na Yao, tutaangalia maendeleo yake akikaa sawa basi anaweza akaingia katika mfumo usajili ujao, ila kwa sasa nafasi yake inachukuliwa na Assinki.
“Yanga tunaimarisha kikosi kutokana na mipango mikubwa tuliyonayo msimu ujao, tunahitaji ubingwa wa Ligi Kuu na kufanya vizuri michuano ya CAF.”
Alisema kwa sasa kila mchezaji atatakiwa kumshawishi kocha Romain Folz ili kuingia katika mfumo wake wa kuwania namba kikosi cha kwanza.
“Kama viongozi tumefanya kazi yetu ya kusajili na sasa tunamuachia kocha aendelee kukitengeneza kikosi cha kuleta ushindani na mataji kwa ajili ya msimu ujao,” kilisema chanzo hicho.
Yanga imeamua kumchomoa Yao, kwa vile imezidisha idadi ya wachezaji wa kigeni ambayo inaruhusu 12 kwa msimu mmoja kwani tayari ina majembe kama Diarra Djigui, Chadrack Boka, Assinki, Duke Abuya, Mohamed Doumbia, Celestine Ecua, Andy Boyeli, Prince Dube, Maxi Nzengeli, Lassane Kouma, Mousa Bella Conte na Pacome Zouzoua. Maana yake kama Yao asingechomolewa kuingia kwa Assinki kungefanya Yanga iwe na watu 13.