Hamdani Said kuandika historia Kombe la Dunia

Mwamuzi msaidizi wa kimataifa wa Tanzania, Hamdani Said ameteuliwa ni miongoni mwa marefa 12 wa Afrika walioteuliwa kuchezesha Fainali za Kombe la Dunia za Vijana chini ya umri wa miaka 17 mwezi Novemba huko Qatar.

Kwa kuteuliwa huko, Hamdani anakuwa mwamuzi wa kwanza wa Tanzania katika historia kuteuliwa kuchezesha fainali za Kombe la Dunia kuanzia zile za wakubwa hadi za vijana kwa Wanawake na Wanaume.

Hamdani ambaye yumo pia katika orodha ya marefa wanaochezesha Fainali za CHAN 2024 zinazoendelea katika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda ni miongoni mwa marefa nane wasaidizi kutoka Afrika ambao wameteuliwa.

Wengine na nchi zao kwenye mabano ni Sirak Mengis (Eritrea), Hamza Naciri (Morocco), Ahmed Dhouiouhi (Tunisia), Salim Alao (Benin), Amos Abegine Ndong B. (Gabon), Elyeh Robleh Dirir (Djibouti) na Joel Wonka Doe (Liberia).

Afrika imetoa marefa wa kati wanne ambao watachezesha fainali hizo ambao ni Jelly Chavani (Afrika Kusini), Hamza El Fariq (Morocco), Tangy Mebiame (Gabon) na Abdou Abdel Mefire (Cameroon).

Fainali za Kombe la Dunia za Vijana chini ya Umri wa miaka 17 zitafanyika Qatar kuanzia Novemba 3 hadi Novemba 27 mwaka huu.