Hospitali ya Rufaa Mkoa Mbeya yapata vifaatiba vya Sh9.6 mil kuboresha huduma

Mbeya. Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Mbeya  imekabidhiwa vifaa vyenye thamani ya  zaidi ya Sh9.6 milioni kwa lengo la kuboresha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wananchi.

Hatua hiyo imetajwa ni sehemu ya kutatua changamoto katika sekta ya afya sambamba na kugusa eneo la elimu kama sehemu ya kurejesha asilimia  10 ya faida yake kwa kila mwaka.

Kauli hiyo imetolewa leo Ijumaa Agosti 22, 2025 na Kaimu Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Lembris  Israel wakati akikabidhi vitanda 20 na mashuka 20 vyenye thamani ya Sh9.6 milioni kwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Beno Malisa katika Hosptali ya Rufaa Mkoa.

Amesema kama wadau wana kila sababu ya  kuunga  mkono juhudi za Serikali katika kuboresha mazingira wezeshi  ya sekta  ya afya, elimu sambamba na majanga mbalimbali nchini

“Leo tumekusanyika hapa Hosptali ya Rufaa Mkoa wa Mbeya, kutoa vifaa hivi magodoro  20 na mashuka 20 vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya Sh9.6 milioni kwa ajili la kulalia wagonjwa kama sehemu ya muendelezo wa kugusa jamii,”amesema.

Amesema utoaji wa vifaa hivyo ni ishara kudhibitisha moja ya ushiriki wao serikalini  na  jamii kama benki inayoongoza nchini kwa kutambua wajibu wao kuhakikisha  huduma  ya afya inaboreshwa na jamii kupata huduma bora.

“Kupitia mfuko wa kusaidia jamii Taasisi  imejikita zaidi  kutatua changamoto  kwenye sekta ya elimu, afya na misaada ya hali na mali katika nyakati ngumu kama za majanga kwa kutenga asilimia 10 ya faida zake kwa kipindi cha miaka kumi sasa,”amesema.

Amesema lengo la kutenga asilimia 10 ni  sehemu ya uwajibikaji kwa jamii inayo wazunguka jambo ambalo limepelekea kuwa kinara wa uwajibikaji kwa mwaka 2025 , hususani  ubora wa huduma na kubaki benki salama zaidi nchini.

Katika hatua nyingine amesisitiza wataendelea  kushirikiana na serikali katika uwekezaji  sekta ya elimu na afya kama sehemu sahihi ya kugusa jamii ya Watanzania.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Beno Malisa amesema taasisi hiyo ya kifedha siyo mara ya kwanza kuwa na mchango kwa Serikali na kutaka kuendelea kuwekeza katika sekta ya elimu na afya.


“Leo tumepokea magodoro 20 na vitanda 20 vitakwenda kuleta chachu katika utoaji huduma,lakini  tuna miundombinu  ya wodi mpya  11 sasa bado wodi 10 zinahitaji  mchango wenu kama itawapendeze mtuongeze,”amesema.

Mjumbe wa Bodi ya Hospitali ya Rufaa Mkoa, Dk Julius Kaijage amesema miundombinu ya hospitali iliyowekezwa na Serikali ya kisasa na kuomba benki hiyo kuendelea kuunga mkono.

“Katika uwekezaji wa miundombinu  ya kisasa tunatarajia kuzindua wodi za wagonjwa  binafsi hivi karibuni, lakini leo Mkuu wetu wa Mkoa utapita kukagua  maboresho yaliyofanywa  na Serikali,” amesema.

Mkazi wa Forest  Chriss Fredy  amesema uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali  umekuwa kimbilio la wagonjwa kutoka maeneo mbalimbali na kupelekea uwepo wa idadi kubwa  kupata huduma tofauti na miaka ya nyuma.

“Tunaona Serikali ya awanu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imefikisha huduma za afya hadi kwenye ngazi za kata na vijiji tafsiri hii ni kutaka kupunguza  vifo visivyo vya lazima hususani kwa wakinamama wajawazito na watoto  wanazaliwa,”amesema.