Kauli za Polepole zawaibua INEC, Nida

Dar es Salaam. Kauli ya aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole, kwamba mifumo ya Chama cha Mapinduzi (CCM) imeunganishwa na ile ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), imewaibua wakuu wa taasisi hizo na kukanusha madai hayo.

Wakuu hao wamebainisha kwamba hakuna mfumo wowote kwenye taasisi zao uliounganishwa na ya chama chochote cha siasa na kwamba jambo hilo si siri, na endapo lingekuwa hivyo lingekuwa tayari limejulikana.

Katika mazungumzo yake aliyoyafanya usiku wa kuamkia leo Agosti 22, 2025, Polepole amedai kwamba mifumo ambayo chama hichoimeijenga, inakiwezesha kupata ushindi hata kabla hawajakwenda kwenye uchaguzi.

“Hii mifumo, mimi nikiwa sehemu ya wasanifu, imeunganishwa kutoka kwenye Chama cha Mapinduzi, imeunganishwa kwenye Nida, imeunganishwa kwenye mifumo ya Tume ya Uchaguzi.

“Ndiyo maana kule chini wanawauliza watumishi wa umma, na hii watumishi wa umma watathibitisha, kule chini kuna watu wanawafuata wanawaambia nipe kadi yako ya kupiga kura, nipe zile namba zako, wanauliza zile namba,” amesema Polepole.

Amesisitiza kwamba wakati mifumo hiyo inaanzishwa, dhamira yake ilikuwa njema, lakini ikishikwa na watu wabaya, dhamira yake ni mibaya kabisa.

“Mtu huyu anayejua mifumo ya kompyuta, aende kuthibitisha mifumo yetu sisi inaenda wapi…kuna liwaya linatoka chama linakwenda Nida, linatoka chama linakwenda Tume ya Uchaguzi,” amesema Polepole.

Akizungumzia tuhuma zilizoibuliwa na Polepole, Mwenyekiti wa INEC, Jaji Jacobs Mwambegele amesema hakuna mfumo wowote wa taasisi hiyo uliounganishwa na chama chochote cha siasa, hususani CCM.

“Hakuna. Sisi ni Tume huru na vitu kama mifumo kuunganisha si vitu vya siri, ukienda tu kitaalumu utajua, ni mfumo gani tuliounganisha na mtu mwingine,” amesema mwenyekiti huyo.

Jaji Mwambegele amesisitiza kwamba hata kama wangekuwa wameunganisha, hiyo inawahakikishiaje ushindi, kwani Tume hiyo inafanya kazi kwa mfumo wa dijitali? amehoji katika majibu yake.

“Kwa maana; je, kura zitapigwa kielekroniki? Kwa hiyo, hakuna kitu kama kuunganisha mifumo ya INEC na chama kingine, lakini nataka nimsikilize anavyozungumza huyo Polepole,” amesema Jaji Mwambegele.

Mwenyekiti huyo amesema mifumo yao haijaunganishwa na chama chochote cha siasa na hata Daftari la Kudumu la Wapigakura wameligawa kwa vyama vyote vya siasa, vinginevyo wangeweza kusema waunganishe katika mifumo yao ili waone.

“Lakini, daftari tumeligawa kwa vyama vyote vya siasa tangu Julai 27, 2025 kwa mfumo kidijitali na mfumo wa hardcopy (nakala ngumu),” amesema.

Jaji Mwambegele amesisitiza kwamba msimamo wa INEC, mjadala unaoendelea kuhusu kuunganisha mifumo, si wa kweli na wananchi hawapaswi kuamini hilo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Nida, James Kaji pia amesema hakuna jambo kama hilo la kuunganisha mifumo, huku akisisitiza Polepole aeleze vizuri kama aliwahi kufanya kazi na mamlaka hiyo huko nyuma.

“Hakuna kitu kama hicho. Ni vema akawaelezea vizuri labda yeye anajua na kama ameshafanya kazi Nida,” ameeleza Kaji alipoulizwa na Mwananchi kuhusu tuhuma zilizoibuliwa na Polepole kuhusu kuunganishwa kwa mifumo hiyo.

Kwa nyakati tofauti, Mwananchi limefanya jitihada za kuwatafuta viongozi wakuu wa CCM akiwemo Katibu Mkuu wa chama hicho, Balozi Emmanuel Nchimbi ambaye simu yake iliita bila kupokelewa, hata alipotumiwa ujumbe mfupi haukujibiwa.

Siyo Dk Nchimbi pekee, pia Mwananchi limemtafuta Katibu wa Itikadi, Uenezi wa Mafunzo wa CCM, Amos Makalla ambaye kama ilivyokuwa kwa Katibu Mkuu, naye simu yake haikupokewa na ujumbe mfupi aliotumiwa haukupata majibu.