TIMU ya Taifa la Madagsacar imeweka rekodi kwa kuwa ya kwanza kutinga nusu fainali ya michuano ya CHAN 2024 baada ya kuifunga Kenya ‘Harambee Stars’ kwa mikwaju ya penalti 4-3 baada ya kutoka sare ya bao 1-1 ndani ya dakika 120 kwenye Uwanja wa Kimataifa wa michezo wa Moi, Nairobi.
Kenya ilianza mechi hiyo kwa kutengeneza mashambulizi mfululizo kupitia kwa Ben Stanley Omondi na Ryan Ogam ambaye alifunga kwenye mechi ya mwisho ya hatua ya makundi dhidi ya Zambia.
Ndani ya dakika 30 za kipindi cha kwanza, Harambee Stars ilipiga mashuti mawili ambayo hata hivyo, hakuna lililolenga lango huku Madagascar ikionekana kucheza kwa tahadhari zaidi.
Majaribio ambayo Kenya ilikuwa ikiyafanya yalijipa mwanzoni tu mwa kipindi cha pili kupitia kwa Alphonce Omija ambaye aliifungia timu yake bao safi.
Hata hivyo, bao hilo lilidumu kwa dakika 21 tu kwani Madagascar ilisawazisha kwa mkwaju wa penalti kupitia kwa Fenohasina Razafimaro.
Katika dakika ya 70, kocha wa Kenya, Benni McCarthy aliamua kufanya mabadiliko mawili kwa mpigo kwa kuwatoa Boniface Muchiri na Ryan Ogam huku wakiingia Edward Omondi na Austine Odongo.
Pamoja na uwepo wa mabadiliko hayo, Kenya ilishindwa kupata bao la pili ndani ya dakika 120 za mchezo huo na kumalizika kwa sare ya bao 1-1. Kenya ilikuwa na umiliki wa mchezo kwa asilimia 51.
Huku ikipiga mashuti 10 na manne yakilenga lango, Madagascar yenyewe ambayo ilionekana kucheza soka la pasi fupi fupi ilipiga mashuti matano huku mawili tu ndio yakilenga lango.
Kenya ilikosa mikwaju miwili ya penalti kupitia kwa Kibwage na mfungaji wa bao Omija, huku wakifunga kupitia kwa Siraji, Sakari na Owino.
Kwa upande wa Madagascar ambao kipa wao aliokoa mkwaju mmoja sawa na yule wa Kenya walifunga kupitia kwa Randriamanampisoa, Rafanomezantsoa, Rakotondraibe na Razafimaro na sasa wanasubiri mpinzani wao baada ya mechi kati ya Uganda na Senegal.