Majaliwa ataka mikakati iendane na mabadiliko teknolojia

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amevisihi vyama vya wafanyakazi barani Afrika, kuweka mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya teknolojia duniani.

Amesema kwa kufanya hivyo kutawawezesha kupunguza hatari ya kupoteza ajira kutokana na ujio wa mashine na matumizi ya teknolojia mpya ikiwemo za akili unde.

Majaliwa ameyasema hayo jijini Dar es Salaam leo Ijumaa, Agosti 22, 2025, alipohutubia Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Afrika (OATUU).

Amesema katika dunia ya sasa, imeshuhudiwa kuwepo kwa mabadiliko yanayochochewa na mapinduzi ya teknolojia ikiwemo matumizi ya akili unde na utandawazi.

“Kuna hatari ya watu kupoteza ajira zao kadri mitambo na mifumo ya kisasa inavyochukua kazi ambazo kwa kawaida zingeweza kufanywa na wafanyakazi.

“Tunapaswa kuweka mpango wa kutoa mafunzo endelevu yanayoendana na mabadiliko ya teknolojia ili kuwaandaa wafanyakazi na aina mpya za ajira zinazojitokeza,” amesema.

Amesema Tanzania imeweka mikakati ya kukabiliana na mabadiliko hayo ikiwemo kuhamasisha matumizi sahihi ya teknolojia mpya na kusisitiza ulinzi wa haki na faragha za wafanyakazi.

“Teknolojia lazima ilinde utu na si kudhoofisha heshima ya kazi,” amesema Majaliwa.

Majaliwa amesema Serikali inathamini na kutambua mchango wa vyama vya wafanyakazi na itaendelea kushirikiana navyo katika kuboresha masilahi ya wafanyakazi.

“Serikali imevipa nafasi vyama vya wafanyakazi uhuru wa kufanya kazi bila kuingiliwa na tunavisihi kuendelea kushauriana na kushirikiana na Serikali ili kuendelea kuboresha maslahi na mazingira ya ufanyaji kazi,” amesema.

Ushirikiano mzuri uliopo baina ya Serikali na vyama hivyo, amesema umeiwezesha Serikali kutekeleza mahitaji yote muhimu ya wafanyakazi, ikiwemo maboresho ya sera, sheria na maslahi ya wafanyakazi.

Ameeleza Serikali itaendelea kuunga mkono jitihada za Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Afrika, ikiwa ni sehemu ya kuenzi jitihada za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ambae ni mwanzilishi wa shirikisho hilo.

Makamu wa Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Afrika (OATUU), Joshua Ansah amesema chama hicho kitaendelea kusimamia na kuhakikisha kinasimamia maslahi ya wafanyakazi Afrika, ili kuhakikisha usawa na maslahi kwa wote.

“Tuendelee kuunga mkono shirikisho letu kwa maslahi mapana ya wafanyakazi Afrika na pamoja tutaendelea kusimamia na kupigania kuboresha maslahi yao,” amesema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la wafanyakazi Kanda ya Afrika Mashariki (ILO), Caroline Mugala ameeleza chama hicho kitaendelea kusimamia umadhubuti na ufanisi wa vyama vya wafanyakazi ili Serikali ziendelee kusimamia maslahi ya wafanyakazi.

“Tunahitaji kuendelea kuwalinda wafanyakazi wetu kutokana na mabadiliko mbalimbali ya kijamii ikiwemo mazingira na teknolojia ni muhimu wafanyakazi waendelee kupewa mafunzo na kuwezeshwa kukabiliana na mabadiliko haya,” ameeleza.

Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) Tumaini Nyamhokya, amesema chama hicho kinajivunia mafanikio yaliyopatikana kwa kupigania haki za wafanyakazi.

Amesema mafanikio hayo yametokana na mahusiano mazuri yaliyojengwa kati ya chama hicho, Serikali na watumishi, jambo lililowezesha kufikiwa malengo tarajiwa.

“Tumetumia kwa kiasi kikubwa njia ya majadiliano na maridhiano katika kufanikisha mahitaji ya wafanyakazi tunashukuru kwa upande wetu Serikali yetu imekuwa sikivu kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakuta wafanyakazi,” ameeleza.