Dodoma/Dar. Mahakama Kuu Masjala Kuu Dodoma imeifuta kesi ya kikatiba ya kupinga uteuzi wa Samia Suluhu Hassan, kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, 2025.
Uamuzi huo umetolewa kutokana na pingamizi la awali lililowekwa na Chama cha Mapinduzi (CCM).
Kesi hiyo imefutwa leo Agosti 22, 2025 na jopo la majaji Joachim Tiganga (kiongozi wa jopo), Everisto Longopa na Griffin Mwakapeje kutokana na kukiuka katiba na kanuni za uchaguzi za CCM, pia tofauti ya majina ya mlalamikaji kwenye kiapo.
Kesi hiyo ilifunguliwa na mwanasiasa mkongwe, Dk Godfrey Malisa, mkazi wa Moshi, mkoani Kilimanjaro, anayejitambulisha kuwa mwanachama wa CCM, dhidi ya Wadhamini wa chama hicho (mdaiwa wa kwanza) na Katibu Mkuu wa CCM (mdaiwa wa pili).
Samia alipitishwa na Mkutano Mkuu wa CCM Taifa, Januari 19, 2025, kuwa mgombea urais katika uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 29, 2025.
Dk Malisa alifungua kesi ya kikatiba kupinga uteuzi huo akidai ni batili kwa kuwa mchakato wake ulikiuka katiba ya CCM na Katiba ya Nchi ya mwaka 1977.
Hivyo, aliiomba Mahakama itamke kwamba haki za msingi, uhuru na wajibu kwa mujibu wa Katiba ya nchi zinazopaswa kufurahiwa na wanachama wote wa CCM na wale wanaonuia kugombea nafasi za uongozi zimekiukwa na wadaiwa.
Pia aliomba Mahakama itamke kuwa, uteuzi wa mgombea urais wa CCM uliofanywa na Kamati Kuu ya mdaiwa wa kwanza, Halmashauri Kuu ya Taifa na Mkutano Mkuu wa Taifa, ni batili tangu mwanzo, haukuwa halali na ulikuwa kinyume cha taratibu.
Vilevile, aliiomba itoe amri kutengua uteuzi wa mgombea urais wa CCM na amri ya kuwalazimisha wadaiwa kufanya upya mchakato wa uteuzi wa mgombea urais kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao.
Kabla ya kesi hiyo kusikilizwa, CCM katika majibu ya maandishi yaliyoungwa mkono na kiapo cha mmoja wa wadhamini, Kapteni George Mkuchika ilikana kukiuka utaratibu ikidai taratibu zote za chama zilizingatiwa, huku ikiibua pingamizi la awali.
Katika pingamizi hilo, iliiomba Mahakama isisikilize kesi hiyo, bali iifute ikibainisha sababu tatu, ya kwanza ni kuwa mlalamikaji alikosea kufungua kesi hiyo kabla ya kufuata utaratibu wa chama kuwasilisha malalamiko yake.
Pili, ilidai kesi hiyo inaungwa mkono na kiapo chenye kasoro za kisheria zisizorekebishika kwa kuwa kimewahusisha watu watatu tofauti. Tatu, kwamba kiapo hicho kimeingiza mambo yasiyotakiwa kuwamo kama vile hoja za kisheria, maoni na hitimisho.
Wakati wa usikilizwaji wa pingamizi hilo, CCM iliwakilishwa na Mawakili Fabian Donatus na Alex Mgongolwa, ambao walidai mlalamikaji alipaswa kutumia njia za ndani ya chama, kwanza kwa kuwasilisha malalamiko yake kwa katibu mkuu.
Pia walidai kiapo kilichounga mkono hati ya madai kina kasoro za kisheria zisizorekebishika.
Mlalamikaji aliyewakilishwa na Wakili Denis Maringo, alipinga sababu za pingamizi hilo akidai mteja wake alifuata taratibu kwa kuwa kabla ya kufungua kesi hiyo alimwandikia barua mwenyekiti wa CCM Taifa, pia kiapo hakikuwa na kasoro.
Mahakama katika uamuzi uliosomwa na Jaji Tiganga kwa niaba jopo, imekubali hoja za pingamizi kuwa kiapo kilichounga mkono hati ya madai kina kasoro ambazo haziwezi kupuuzwa.
Jaji Tiganga amezitaja kasoro hizo kuwa, aliyekula kiapo hicho ana majina matatu tofauti, jambo ambalo halikubaliki kisheria.
Amebainisha jina la aliyekiandika ni Dk Godfrey Fatael Mlamie Malisa, huku aliyesaini mwisho wa kiapo ni Godfrey Fatael Mlamie Malisa (siyo Dk) na aliyeapa kwa Kamishna wa Viapo ni Godfrey Fatael Malisa (hakuna Dk wala jina Mlamie).
”Hii inaonyesha aliyeandika kiapo siyo aliyesaini kiapo hicho na wala siye aliyeapa mbele ya kamishna wa viapo. Inaonyesha ni watu watatu tofauti na mapungufu haya ya kisheria hatuwezi kuyafumbia macho, kwa sababu yanafanya kiapo hiki kukosa sifa ya kiapo,” amesema.
Jaji Tiganga amesema kwenye kiapo mdai alitoa malalamiko, lakini pia akatoa hitimisho la malalamiko hayo jambo ambalo halikubaliki kisheria akieleza alichotakiwa kuwasilisha ni maombi pekee.
Kuhusu hoja ya kutokufuata taratibu ndani ya chama, Jaji Tiganga amesema sheria inaitaka Mahakama kujiridhisha kama kabla ya kufungua kesi ya kikatiba mdai amepitia ngazi zote zinazotoa nafuu ya kupata haki yake.
Amesema mawakili wa wadaiwa waliwasilisha kanuni za uteuzi wa wagombea wa uongozi katika vyombo vya dola, ambazo zinamtaka mtu ambaye hataridhishwa na mchakato wa kuwapata wagombea hao kuandika barua ya malalamiko kabla, wakati na baada ya kura za maoni ili hatua zichukuliwe.
Amesema katika kesi hiyo Mahakama imejiridhisha kuwa mdai (Dk Malisa) hakufuata utaratibu huo.
Amesema kumbukumbu zinaonyesha Februari 12, 2025 mdai alimwandikia barua mwenyekiti wa CCM kumweleza nia yake ya kukishtaki chama na kuishtaki Bodi ya Wadhamini wa chama hicho.
Jaji amesema hayo hayakuwa malalamiko ya kukiukwa kwa katiba ya chama hicho wala ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kumteua Rais Samia kuwa mgombea urais kupitia chama hicho.
Hivyo, amesema mdai kabla ya kwenda mahakamani alitakiwa kufuata masharti ya kanuni hizo za CCM ambazo pia zipo kwenye katiba ya chama hicho ili hatua zichukuliwe kutokana na kukiukwa kwa katiba ya chama.
“Kutokana na kasoro ya kiapo na kutofuatwa taratibu zilizowekwa na chama katika kuwasilisha malalamiko pale mtu anapokuwa na malalamiko, Mahakama inalifuta shauri hili. Kila upande utabeba gharama za kesi,” amesema.
Katika kesi hiyo, Dk Malisa alidai utaratibu uliotumika kumteua Samia kuwa mgombea urais umemnyima haki ya kushiriki kikamilifu katika masuala ya kisiasa na haki za kidemokrasia.
Alidia haki hizo zinatolewa na Katiba ya nchi, kwa mtu anapotaka kugombea nafasi mbalimbali za kisiasa ndani ya chama kilichosajiliwa.
Vilevile alidai ulikiuka ibara ya 103(12)(b) ya katiba ya CCM ambayo inaitaka kamati kuu kupendekeza majina matatu ya wagombea wa nafasi ya urais.
Alidai taratibu za mkutano zilikiuka ibara ya 39(1)(a), (b), (c), (d), na (e) za katiba ya CCM na misingi ya haki asili (haki ya kusikilizwa, kanuni dhidi ya upendeleo), pamoja na kanuni za kura ya siri.
Alidai hakuweza kutumia njia zinazopatikana ndani ya vikao vya chama hicho kwani haziwezi kuwa za haki au za uhalisia kwa sababu walewale wanaolalamikiwa ndio wangeketi kusikiliza malalamiko yake.