WAKATI vigogo vya soka vikiendelea kutambiana kwa sajili zao, kuna watu wanaitwa Mashujaa wanafanya usajili mzuri sana wa wachezaji wazawa.
Ndiyo tunakumbuka hapa kijiweni Mashujaa inamilikiwa na Jeshi la Wananchi Tanzania na kama ilivyozoeleka timu za majeshi huwa kwa asilimia kubwa zinatoa fursa kwa watoto wa nyumbani kwa maana ya wachezaji wazawa.
Sasa kama husajili wachezaji wa kigeni basi hakikisha hao wazawa unaowasajili wana ubora na wanaweza kuipandisha kiwango timu siyo wawe wa kutimiza idadi tu kwenye kikosi.
Kijiwe tumeushtukia usajili wa Mashujaa katika dirisha linaloendelea la usajili na tumegundua jamaa wanasajili wazawa ambao kama benchi la ufundi likiwatumia vizuri msimu ujao, yale mambo ya kuishi na presha ya vita ya kuwania kubaki Ligi Kuu hayatokuwepo.
Fikiria winga moja ya Mashujaa msimu ujao itakuwa na Seleman Bwenzi na upande mwingine atakuwepo fundi wa mpira, Salum Kihimbwa ambaye Maafande hao wamemsajili akitokea Fountain Gate.
Hao mawinga wawili jukumu lao litakuwa kumlisha straika wa mpira, Ismail Mgunda lakini nyuma yao wana viungo kama Omary Omary, Idrisa Stambuli, Samuel Onditi na Yusuph Dunia fikiria wapinzani watakutana na ushindani wa namna gani hapo.
Pale mbele kumbuka kwenye benchi watakuwa na Jafari Kibaya, Crispine Ngushi, Seif Karihe, David Ulomi na kina Cheda yaani hapo anayetoka ni moto na anayeingia ni moto.
Unapofanyika usajili mzuri kama huo, mtu ambaye anakuwa anawekwa katika mtego ni kocha mkuu maana tayari uongozi unakuwa umeshamaliza jukumu lake na sasa linabakia la kwake yeye na wenzake katika benchi la ufundi kuhakikisha timu inafanya vizuri.
Kimsingi Mzee wangu Salum Mayanga ana kazi kubwa ya kuhakikisha Mashujaa inafanya vizuri kwani hakuna cha kujitetea maana wachezaji wazuri ameshapewa kazi imebaki kwake kuwatumia.