Mkurugenzi wa Kampuni ya Chocolate Princess,Mboni Masimba, amemrudisha jukwaani mkongwe wa Taarabu nchini, Mwanahawa Ally aliyetangaza kustaafu kuimba mwaka jana.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mboni amesema, anatarajia kufanya tamasha la mkesha wa muziki wa taarabu litakalohusisha wakali wasanii wa muziki huo nchini akiwemo Mwanahawa Ally, Agosti 28 kwenye Viwanja vya Posta, Kijitonyama huku mgeni rasmi anatarakiwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila.
Mbona amewataja wasanii wengine watakaotoa burudani siku hiyo ni; Khadija Kopa, Sabah Salum Muchacho, Khadija Yusuf, Isha Ramadhani ‘Isha Mashauzi’, Mzee Yusuf, Zanzibar One, Leila Rashid na East Afrika Melody.
“Tamasha hilo ni bure limebeba kauli mbiu ya
‘Wanamwambao tunatamba na Mama’, hili ni tamasha la kishua lenye ladha ya taarabu ya kipekee tutaanza saa 10 jioni hadi majogoo,
Tamasha hilo linatarajiwa kuvuta mashabiki lukuki kutokana na orodha ndefu ya wakongwe wa taarabu akiwemo Khadija Kopa, East Afrika Melody, Sabah Muchacho, Khadija Yusuf, Isha Ramadhani ‘Isha Mashauzi’, Mzee Yusuf, Zanzibar One na Leila Rashid, na Bi Mwanahawa Ally ambaye alitangaza kuacha muziki ila tumemuomba siku hiyo aje atoe burudani na uzuri afya yake kwa sasa inaendelea vizuri na hii itakuwa ni moja ya mazoezi kwake kwani burudan ni afya kwa binadamu,” amesema Mboni.
Kwa upande wa Mzee Yusuf, amesema taarabu ni muziki unaoibeba Tanzania kimataifa na kufafanua haya;
“Taarabu ni muziki wa kipekee, ukienda dunia nzima, ukitaja taarabu watu wanaielekeza Tanzania. Muziki huu unaweza kuchezwa na rika zote bila kubagua. Tamasha hili limekuja kwa wakati muafaka.”