Mchengerwa Atoa Wito kwa Watumishi wa Afya Kuhudumia Wananchi kwa Upendo
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Mohammed Mchengerwa, amewataka wataalamu wa sekta ya afya nchini kufanya kazi kwa weledi, kusikiliza wananchi na kuwahudumia kwa moyo wa huruma na upendo.
Wito huo umetolewa leo, Agosti 22, 2025, wakati wa ziara yake ya kikazi wilayani Bagamoyo, mkoani Pwani, ambapo alikagua miradi ya maendeleo ikiwemo ukarabati wa Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo na ujenzi wa Bweni la wanafunzi wenye mahitaji maalum katika Shule ya Msingi Nia Njema.
Katika ziara hiyo, Mhe. Mchengerwa pia alizindua jengo jipya la wagonjwa wa nje (OPD) katika hospitali hiyo, na kutoa pongezi kwa watumishi wa sekta ya afya kwa kazi nzuri wanayoifanya katika kuwahudumia wananchi.
“Kada ya afya ni kada ya kujitolea sana. Hivyo, niwaombe muendelee na moyo huo huo wa kuwahudumia wananchi kwa upendo na kujali utu wao,” alisema Mchengerwa.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi wa ukarabati wa Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo, Mganga Mkuu wa Wilaya, Dkt. Kandi Lussingu, alisema kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo ilipokea shilingi milioni 900 kutoka Serikali Kuu kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu chakavu ya hospitali hiyo.
Alisema kazi zilizofanyika ni pamoja na ukarabati wa majengo ya huduma ya mama na mtoto (RCH), jengo la utawala, wodi tatu, stoo ya dawa, nyumba ya watumishi, jengo la OPD ya zamani, wodi ya wazazi (ghorofa moja) na njia za watembea kwa miguu (walkways).
Mradi huo umetekelezwa kwa kutumia mfumo wa Force Account.