OFISI YA MAKAMU WA RAIS YAAANDAA KONGAMANO LA UCHUMI WA BULU

…………….

Ofisi
ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI)
imeandaa kongamano la kitaifa la uchumi wa buluu ili kuwaleta pamoja wadau
kujadili dira ya sekta hiyo.

Kongamano hilo
litafanyika jijini Dar es Salaam Septemba 10 hadi 11, 2025 na kuwashirikisha washiriki zaidi ya 250 kutoka sekta za
uchumi wa buluu za serikali, vyuo vikuu, vijana, wanawake na taasisi zisizo za
kiserkali.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Agosti 22,
2025, Naibu Katibu Mkuu (Muungano) Ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Abdallah Hassan
Mitawi amesema kongamano ni utekelezaji wa Sera ya Uchumi wa Bluu (2024)
inayotekelezwa na Ofisi ya Makamu wa Rais.


Alisema Serikali imeweka dhamira ya dhati katika
kuhakikisha kuwa rasilimali za bahari, maziwa na mito zinatumika kwa tija ili
kuchangia kikamilifu uchumi wa mwananchi mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.


“Sote tunatambua kuwa uchumi wa buluu
unaongeza ajira kwa vijana na kuboresha ustawi wa wananchi bila kuathiri
mazingira,” alisema Mitawi.

Aidha, alisema matarajio ya kongamano hilo ni
kuziainisha fursa zilizopo katika sekta hiyo na kuonesha kwa namna gani
zimebadili maisha ya wananchi na uchumi kwa ujumla.

Aliongeza kuwa kongamano
hilo litakuwa ni chombo cha utekelezaji wa kisera kinachowezesha mjumuisho wa
waau na kutoa mrejesho wa moja kwa moja kwa Serikali kuhusu fursa na mikakati
ya kitaifa.

Hivyo, alisema kupitia
maazimio yatakayofikiwa, Serikali itaandaa mpango kazi mahsusi wa utekelezaji
wa sera, kuvutia uwekezaji, kukuza ajira za vijana na wanawake pamoja na
kulinda mazingira ya majini.

Halikadhalika, Naibu Katibu Mkuu Mitawi alisema
tayari Idara ya Uchumi wa Bluu imeanzishwa chini Ofsi ya Makamu wa Rais kwa
lengo la kuratibu sekta zote zinazohusika na uchumi wa buluu.

Pamoja na
hatua hiyo, ili kufanikisha utekelezaji wa Sera hii kikamilifu, kunahitajika
ushiriki wa wadau wote katika ngazi zote, ikiwemo sekta binafsi, Asasi za
Kiraia na Washirika wa Maendeleo.