Geta. Kufuatia madai ya kutekwa na watu wasiojulikana kwa mwimbaji wa nyimbo za injili Elisha Juma mkazi wa Mtaa wa Kadisi, Kata ya Katente wilayani Bukombe mkoani Geita, Jeshi la polisi mkoani humo limesema linafuatilia na kuchunguza tukio hilo.
Taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita Safia Jongo na kuchapishwa kwenye mtandao wa instagram wa jeshi hilo, imeeleza kuwa mwimbaji huyo wa nyimbo za injili alichukuliwa Agosti 19,2025 saa 10 jioni akiwa Studio ya Mas iliyopo Mtaa wa Kilimahewa, Kata ya Bulangwa wilayani humo.
Kamanda Jongo amesema Juma alichukuliwa na watu watatu ambao hawakufahamika waliokuwa na gari yenye rangi nyeupe ambayo pia haikufahamika usajili wake na kuondoka naye kusikojulikana.
Amesema taarifa ya kutekwa kwa mwimbaji huyo ziliripotiwa Agosti 21, 2025 saa saba mchana katika Kituo cha Polisi Bukombe.
Amesema licha ya kuwa wakati mwimbaji huyo anachukuliwa, watu wengine waliokuwepo katika studio na mazingira hayo hawakuweza kutoa taarifa hadi pale zilipowasilishwa kituoni hapo jana.
Amesema tayari hatua za uchunguzi juu ya tukio hilo zimeanza mara moja na kutoa wito kwa wananchi kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa sahihi na kwa wakati kuhusiana na tukio lolote la uhalifu ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa.
Jeshi hilo pia limewataka wananchi kuwa watulivu wakatii wakiendelea na uchunguzi wa tukio hilo.
Mapema Agosti 21, 2025 zilisambaa taarifa kwenye mtandao ya kijamii za kutekwa na watu wasiojulikana mwimbaji huyo anayetambulika zaidi kwa nyimbo za injili igeuzayo roho.
Taarifa hizo zilidai watu hao walifika studio alikokuwa anarekodi, wakisema wanapenda nyimbo zake kwa hiyo wanahitaji kumuona na yeye alitoka kuonana nao na wakatokomea naye kusikojulikana.