Same. Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amesitisha kwa muda wa siku 14 shughuli zote za matumizi ya ardhi kwenye eneo lenye ukubwa wa ekari 2,787 zilizopo katika Kijiji cha Marwa, Kata ya Ruvu, Wilaya ya Same mkoani humo, kufuatia mgogoro uliopo baina ya wakulima na wafugaji.
Mkuu huyo wa mkoa amesema uamuzi huo umechukuliwa ili kutoa nafasi kwa Serikali kuchunguza kwa kina chanzo cha mgogoro huo na kutafuta suluhu ya kudumu itakayoweze
sha pande zote mbili kufanya shughuli zao bila migongano.
Babu amesitisha shughuli hizo jana wakati alipokwenda kwenye Kijiji hicho kwa ajili ya kushughilikia mgogoro huo wa ardhi ambao umekuwa ukihatarisha amani na usalama kwa wananchi wa eneo hilo.
Kufuatia hali hiyo, RC Babu ameunda kamati ya wataalamu waliobobea katika masuala ya ardhi, mifugo, kilimo na sheria kwa ajili ya kufanya tathmini ya kina kwa muda wa siku kumi na nne ili kuleta mrejesho na kuona hatua zitakazochukuliwa.
“Katika kipindi hiki cha wiki mbili wafugaji kwenye hili eneo la ekari 2,787 wasiguse kuanzia leo na nyie wakulima katika eneo ambalo mmegawana gawana nalo lisimame kwa kipindi cha wiki mbili,” amesema RC Babu.
Amesema; “Na mimi nitapiga mahali nipate majibu na nitarudi tena mwenyewe hapa kwenye mkutano kama huu niseme tumeamua nini. Lakini, wataalamu wangu watatembelea katika eneo hili.
“Ni lazima tuwe na utaratibu ambao utatufikisha mahali ambapo wakulima na wafugaji hawataleta manung’uniko, mrudi muwe Watanzania. Pia mrudi muwe wanakijiji wa Marwa, lazima muwe kitu kimoja, amani na utulivu uwepo ilivyokuwa zamani.”
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Same, Abdallah Mnyambo amewataka wananchi kudumisha utu na mshikamano katika maisha ya kila siku ili kuhakikisha amani na maendeleo yanakuwepo katika maeneo hayo.
“Maagizo yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa kuhusu wataalamu watakaokuja basi viongozi wenye busara kwa wakulima na viongozi wenye busara kwa wafugaji wote mkae mahali pamoja,” amesema.
Amesema: “Yote yatakayoamuliwa baina yenu nyie na timu hizo mbili pamoja na wataalamu ndiyo yatakayokuwa maamuzi ya Serikali, yule atakayeenda kinyume na hilo asijekulaumu au kulalamika.”
Awali akizungumza mmoja wa wafugaji katika mkutano huo, Ngenesa Sandela amesema chanzo cha mgogoro huo ni mafuriko yaliyotokea mwezi Mei mwaka huu, yaliyosababisha zaidi ya wakulima 600 kukosa maeneo ya kulima.
Mmoja wa wakulima wa kijiji hicho, Grace Joseph, amesema suluhu ya mgogoro huo itasaidia kukuza uchumi na kuboresha ustawi wa wakazi wa Kijiji cha Marwa.