SELF Microfinance kufanyia kazi vipaumbele 8, kufikia malengo Dira ya Taifa

Wananchi wengi zaidi watafikiwa na SELF Microfinance [Mfuko wa SELF] ambao tayari umeainisha vipaumbele vinane vya utekelezaji vitakavyoendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 – 2050.

Hatua hiyo inalenga kuimarisha huduma zinazotolewa na Mfuko huo ulio chini ya Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Fedha, ulioanzishwa mwaka 2015.

Mwenyekiti  wa Bodi Paul Sangawe kwa mara ya kwanza na waandishi wa habari Mkoani Arusha, tangu alipoteuliwa kwa awamu ya pili na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuiongoza bodi hiyo.

Ametaja vipaumbele watakavyosimamia ni pamoja na ufunguzi wa matawi mapya, uelimishaji jamii, ongezeko la mtaji pamoja na uimara wa taasisi hiyo iliyo chini ya Serikali kupitia Wizara ya Fedha.

Kipaumbele kingine ni kufanya mapitio ya viwango vya riba zake ziwe rafiki zaidi kwa wananchi, kuongeza gawio kwa Serikali na kuimarisha ushirikiano wa wadau.

Mfuko wa SELF umedhamiria pia kuimarisha taasisi kupitia ushirikiano wa wafanyakazi na wateja na kuwa na Mpango Mkakati wa Muda Mrefu.

Mpango huo utazingatia maeneo yaliyoainishwa katika Dira ya Maendeleo ya Taifa na yatakayoainishwa katika Mpango wa Taifa wa Muda Mrefu [LTPP] na mipango ya kimataifa.

“Huduma za ki-fedha ni mojawapo ya kichocheo muhimu cha mageuzi ya ki-uchumi Tanzania kwa mujibu wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025 – 2050,” amesema.

Ameongeza “Ni muda mwafaka wa kila taasisi kujipanga vema kuona namna gani itaweka mipango yake ili iendane na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2050,” amesema.

Amesema kwa  uzinduzi wa dira ile tafsiri yake mojawapo ni pamoja na mashirika, taasisi za umma kujipanga upya kwa kuzingatia malengo na vipaumbele ambavyo vimeainishwa katika dira.

“Kwa hiyo pamoja na mafanikio ambayo [SELF] tumepata, tunadhani huu ndiyo muda wa kujipanga, kufanya jitihada ili kuhakikisha mfuko unaendelea kuhudumia wananchi kwa ufanisi,” amesisitiza.

Amefafanua “Lakini pia vile vile, kufikia malengo na vipaumbele ambavyo vimeainishwa katika dira.

Awali Afisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa SELF Santieli Yona amesema jukumu kubwa la kwanza walilonalo ni kutoa mikopo kwa wajasiriamali wadogo ili waweze kuinuka ki-uchumi.

Amesema  pia wanalo jukumu la kutoa mikopo kwa taasisi za fedha ambazo zinalenga kutoa huduma za ki-fedha kwa wananchi katika ngazi ya chini kabisa ya jamii.

“Tuna jukumu kubwa la kujenga uwezo wa wajasiriamali ki-biashara, tangu tumeanza 2015 hadi sasa, tumefanikiwa kutoa mikopo zaidi ya TZS 397 Bil,” amesema.

Ameongeza “Wananchi 183,381 wamenufaika na kati ya hao 53% ni kundi la wanawake,”.