SERIKALI KUGHARAMIA MAZISHI YA WALIOFARIKI KATIKA AJALI YA MGODI NYANDOLWA.

:::::::

NA.MWANDISHI WETU – NYANDOLWA SHINYANGA

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge na Uratibu Mhe. William Lukuvi, amemfikishia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, salamu za pole kufuatia ajali ya kufukiwa kwa mafundi katika Mgodi wa Dhahabu wa Nyandolwa, iliyotokea tarehe 11 Agosti 2025 katika Mkoa wa Shinyanga.

Waziri Lukuvi ameeleza kuwa Serikali imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za ajali hiyo, na kwa niaba ya Rais Samia, ametoa pole kwa familia zilizopoteza wapendwa wao katika tukio hilo la kusikitisha. Aidha, ameeleza kuwa Serikali itagharamia kikamilifu gharama za mazishi kwa waathirika wa ajali hiyo pamoja na matibabu kwa waliofikwa na tukio hilo.

Akizungumza na wanandugu wa marehemu na wale waliokwama mgodini, Mhe. Lukuvi amewatia moyo na kuwahakikishia kuwa Serikali ipo pamoja nao katika kipindi hiki kigumu. Ametoa wito kwa timu za uokoaji kuongeza juhudi na kasi ya uokoaji ili kuwaokoa mafundi waliokwama kwa haraka na usalama zaidi.

“Tunaamini kuwa kazi kubwa imefanyika lakini bado tunahitaji jitihada zaidi. Serikali inatambua uzito wa tukio hili na itaendelea kutoa ushirikiano wa karibu kwa kuhakikisha kila jitihada zinafanyika kwa ufanisi,” amesema Lukuvi.

Kwa upande wake, Msimamizi wa Mgodi huo, Fikiri, ameiambia Serikali kuwa ndani ya kipindi cha siku tatu hadi nne zijazo, zoezi la kuwaokoa wahanga waliokwama litakuwa limekamilika. Ameeleza kuwa vifaa vya kutosha vimeletwa eneo la tukio na wataalamu wanaendelea na kazi kwa umakini mkubwa kuhakikisha mafanikio ya haraka.

Kabla ya kuwasili katika eneo la mgodi, Mhe. Lukuvi alifanya ziara katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, ambapo alipokea taarifa ya kina kuhusu maendeleo ya sekta ya madini katika mkoa huo pamoja na hali ya sasa ya shughuli za uokoaji zinazoendelea katika mgodi wa Nyandolwa.

Akizungumza kwa niaba ya ndugu wa wanasubiri waliofukiwa na kifusi Bw.Furaha Enock aliishukuru Serikali kwa namna ilivyoratibu zoezi na inavyowahudumia katika kipindi chote toka tukio kutokea na kueleza kuwa imefanya jambo la kipekee, la heshima na la uungwana kuwashika mkono na kuhudumia kwa hali na mali na kuwasihi wanandugu kuendelea kuwa na utulivu.

“Kipekee ninaipongeza Serikali Yetu imetufanyia wema na imetupa faraja kwa namna wanavyoratibu tukio zima, tunakosa neno zaidi ya Asante sana kwa Rais Dkt. Samia pamoja na uongozo wake wote,” alisema Enock

AWALI

Ziara ya Waziri Lukuvi ni sehemu ya juhudi za Serikali za Uratibu na kutoa maelekezo kwa karibu katika kipindi hiki cha majonzi, huku ikilenga kuimarisha utendaji wa shughuli za uokoaji na kuhakikisha haki na heshima kwa waathirika wote wa ajali hiyo.










 =MWISHO=