Unguja. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji Zanzibar, Shariff Ali Shariff amesema sekta ya viwanda ndio suluhisho pekee kwa vijana kuekeza nguvu zao katika kuleta maendeleo ya nchi.
Hayo ameyasema leo Ijumaa Agosti 22, 2025 wakati akifungua majadiliano ya kampuni za uwekezaji na utengenezaji katika sekta ya viwanda yanayolenga kufungua fursa za uzalishaji na kuunganisha fursa kikanda na kyalifanyika Mjini Unguja.
Amesema, mpango wa majadiliano hayo sio tu kuleta uwezeshaji wa uwekezaji badala yake unalenga kutoa utaalamu wa kiufundi na uhusiano wa kimataifa ili kuwasaidia kuongeza ushindani wa biashara zao.
“Sekta ya viwanda inaweza kuwa suluhisho kwa vijana wa nchi hii kufikia maendeleo na kufungua milango ya nchi kama ilivyo kwa upande wa China ambao nchi yao inategemea zaidi sekta hiyo katika kuendesha nchi yao.
“Natoa changamoto ya kufikiri kwa ujasiri kuwa tusiiangalie Zanzibar kama soko la walaji bali ni kitovu cha uzalishaji ya mauzo ya nje hivyo tuchangamkie fursa za Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika (AfCFTA) ili kuiweka katika kitovu cha mageuzi ya viwanda,” amesema.
Pia, amesisitiza kuwa kufungua uwezo wa uzalishaji kunahitaji juhudi za pamoja kufikia dira ambayo inaweza kuleta mageuzi yenye ushindani wa viwanda, kutengeneza ajira kwa vijana na kuongeza ustawi wa mauzo unaojumuisha wananchi kutoka maeneo mbalimbali.
Ameeleza, kufanyika kwa majadiliano hayo kisiwani hapa itafungua njia mpya kwa watengenezaji wa ndani kuzichangamkia fursa hizo kwa kuongeza tija, kupitisha uvumbuzi na kupata viwango vya ubora vya kimataifa.
Amebainisha kuwa, kwa sasa Serikali inahitaji kuwekeza katika uzalishaji wa viwanda kwa kusarifu mazao ya baharini na viungo ili kuongeza thamani, mazingira hayo yawe mazuri na ndio sababu ya kuanzisha maeneo maalumu kwa ajili ya viwanda.
Licha ya mafanikio mbalimbali yaliyopatikana katika sekta hiyo bado inakabiliwa na changamoto ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa fedha nafuu, teknolojia ya kisasa, nishati ya uhakika na wafanyakazi wenye ujuzi unaolenga viwanda vya hali ya juu.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (Zipa), Saleh Saad Mohamed amesema sekta ya viwanda ni injini inayobadilisha malighafi kuwa bidhaa za thamani kutengeneza ajira nzuri, kuibua uvumbuzi, na kuongeza uwezo wa kuuza bidhaa nje.
Amesema, Serikali imeweka kipaumbele katika maendeleo ya viwanda kama njia ya kimkakati ya kukuza uchumi na kuzalisha ajira kupitia mipango kama vile maeneo maalumu ya kiuchumi na bustani za viwanda.
“Zipa imejitolea kutoa mazingira yaliyo na miundombinu ya kisasa, taratibu zilizorahisishwa na motisha za ushindani ili kusaidia watengenezaji wetu,” amesema Mohamed.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Shear Illusion, Shekha Nassor amesema wawekezaji wengi kisiwani hapa wanakabiliwa na ukosefu wa masoko ya ndani jambo ambalo linasababisha gharama za usafirishaji wabidhaa zao.
Hivyo, ametoa wito kwa Serikali kuunga mkono jitihada za uendelezaji na uzalishaji wa masoko kwani hiyo ndio miongoni mwa changamoto inayowakabili.