Dar es Salaam. Tuna ahamu matunda yenye vitamini C, husaidia kuimarisha kinga ya mwili na kuharakisha uponaji kwa haraka.
Hata hivyo, ulishawahi kujiuliza siku ukikosa machungwa ambayo wataalamu wa masuala ya afya, wanatueleza kuwa yamesheheni vitamin C, unaweza kutumia matunda gani ambayo yatakusaidia kupata vitamin C kwa wingi?
Jibu hili hapa, matunda kama mapera, yatakupa vitamin C ya kutosha.
Ofisa mtafiti mwandamizi kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC), Medina Wandella, anasema moja wapo ya faida ya kula matunda yenye vitamini C, ni kuimarisha kinga ya mwili na kupunguza hatari ya maambukizi ya magonjwa mbalimbali ukiwamo ugonjwa wa Uviko-19.
” Japokuwa hakuna ushahidi wa moja kwa moja wa matumizi ya matunda yenye vitamini C kwa wingi kuzuia au kutibu Uviko- 19, matunda yenye vitamin hizo yanaweza kutumika kuboresha kinga ya mwili pamoja na kupunguza baadhi ya dalili zinazotokana na maambukizi ya Uviko-19,’’ anasema.
Anafafanua kuwa faida nyingine ya ulaji wa matunda yenye vitamini C, ni kwamba yana virutubishi vingi muhimu ikiwemo, vitamini A, D na madini ya kalisi na manganizi ambayo ni muhimu katika kuimarisha kinga ya mwili.
Wandella anafafanua kuwa kutumia matunda halisi ni bora zaidi kuliko kutengeneza juisi, kwani mtumiaji atapata faida nyingine zilizopo katika tunda husika kama vile nyuzi nyuzi .
Anasema endapo matunda hayo yatachemshwa kuna uwezekano mkubwa wa kupoteza vitamini C iliyopo, hivyo inashauriwa kula matunda au kunywa juisi bila kuchemsha.
“Inashauriwa kula matunda hayo mara kwa mara kwani vitamini C ni kati ya vitamini ambazo huyeyushwa na maji na haihifadhiwi mwilini kwa muda mrefu” anasema.
Hata hivyo anashauri watu kutumia matunda hayo kwa kiasi, kwani yana tindikali ambayo huweza kuleta madhara mwilini.
Matunda mengine yenye vitamin C kwa wingi ni pamoja na mananasi, maembe, limao na a machenza.