Tanzania imeungana na Kenya zikiwa nchi wenyeji kutupwa nje ya fainali za Mataifa Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), baada ya kupoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Morocco kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Bao la dakika ya 63 likifungwa na mshambuliaji Oussama Lamlioui akipokea pasi ya kiungo Youssef Belammari limetosha kusitisha matumaini ya Tanzania kubeba taji hilo ikiishia hatua ya robo fainali.
Tanzania itajilaumu juu ya ubora wa safu yake ya ushambuliaji iliyoshindwa kutumia nafasi zilizotokana na makosa ya walinzi wa Morocco kwenye mchezo huo.
Licha ya Tanzania kutawala mchezo huo kwa vipindi vyote viwili, lakini mashambulizi yake yalikosa nguvu mbele ya ukuta wa Morocco.
Nafasi mbili kubwa ambazo Tanzania itazijutia ni Ile ya dakika za mwisho wa kipindi cha kwanza ambapo mshambuliaji Clement Mzize akitazamana na kipa wa Morocco ameshindwa kuchagua sehemu nzuri ya kufunga na kupiga mpira hafifu.
Kiungo Mudathir Yahya katika dakika ya 70 shuti lake lilitoka nje kidogo wakati Tanzania ikifika vizuri kwenye lango la Waarabu huku mshambuliaji Nassoro Saaduni aliyeingia kipindi cha pili akipoteza nafasi nzuri dakika ya 83.
Kutolewa kwa Tanzania linakuwa pigo la pili kwa wenyeji wa fainali hizo kutolewa ndani ya siku moja ambapo mapema Kenya ilitangulia kung’olewa kwa matuta baada ya timu hizo kumaliza dakika 120 zikiwa sare ya kufungana bao 1-1.