Mwanza. Zaidi ya washiriki 500 na wengine 100 kutoka nchi za nje wanatarajiwa kushiriki maonesho ya 20 ya Biashara kwa lengo la kufungua fursa kwa wafanyabiashara wa kada zote Afrika mashariki, yatakayofanyika katika viwanja vya Nyamagana mkoani Mwanza.
Maonesho hayo yataratibiwa na Taasisi ya Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) Mkoa wa Mwanza ambayo yatafanyika tarehe 29 Agosti hadi 7 Septemba 2025 na yatafuguliwa rasmi na Mkuu wa Mkoa Mwanza, Said Mtanda.
Washiriki wanaotarajiwa kuhudhuria maonesho hayo ni 500 na wengine 100 kutoka mataifa mbalimbali ambapo yakitarajiwa kufikia watembeleaji 250,000 kutoka ndani na nje ya nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa TCCIA, Mkoa wa Mwanza, Gabriel Kenene amesema yatafungua fursa kwa wafanyabiashara, wakulima, wenye viwanda, na wajasiliamali ili waweze kujulikana na kutanganza bidhaa zao.
“Tunatarajia kuwa na washiriki zaidi ya 500, wakiwemo wafanyabiashara, viwanda vikubwa na vidogo, wawekezaji, taasisi za kifedha na wabunifu wa teknolojia. Hii ni fursa kubwa ya kuunganisha wajasiriamali, kukuza masoko na kuvutia uwekezaji mkubwa katika Kanda ya Ziwa,” amesema Kenene.
Kanene amesema kutakuwa na bidhaa za mashine na teknolojia, bidhaa za ujenzi thamani za nyumbani na ofisini, bidhaa za kilimo na mifugo, bidhaa za usindikaji na vinywaji bidhaa za hoteli na utalii, sanaa na kazi za mikono, bidhaa za mawasiliano ya habari.
Amesema watakaotembelea na kushiriki maonesho hayo wataongeza mtandao wa kibiashara na teknolojia na kuongeza uzoefu katika biashara na shughuli mbalimbali za maisha.
“Mfano kuna wamama ambao ni wajasiriamali wadogo bidhaa nyingi ambazo zilikuwa zinauzika kwenye supermarket lakini leo zinatoka kwa hawa wajasiriamali wa hapa nchini, hii ni kwa sababu walifika na kushiriki uzoefu na kuweza kusafirisha bidhaa zao kwenda nje,” amesema.
“Kuna makampuni ambayo yalitoka nje, walipofika hapa walionyesha bodhaa zao walitafuta mawakala na baada ya kupata mawakala leo hii ni matajiri wakubwa na walipakodi nchini,” ameongeza.
Akizungumzia maonyesho ambayo yalifanyika mwaka jana ambayo yalikuwa na na washiriki washiriki walikua 220 na 60 kutoka nje na wengine waliotembelea maonesho hayo walikua zaidi ya watu 140,000, amesema kuna changamoto ambazo zilizojitokeza, zimepata utatuzi.
“Kwenye mradi wetu tulionao huwa tunautaratibu kwa wanaoshiriki huwa wanatoa ushauri na maoni na changamoto kwa hivyo changomoto zilizojitokeza mwaka jana tumeziboresha kwa kiasi kikubwa ikiwemo matenti ambayo hayakuwa na ubora na mpangilio wa maonyesho hayo,” amesema.
Ametoa wito kwa wakazi wa Mwanza na mikoa jirani kuchangamkia fursa hii kwa kushiriki na kujifunza mbinu mpya za biashara.
“Tunawakaribisha kuja kujifunza na kubadilishana mbinu mbalimbali za kibiashara kutalii kwa kuona wanayama hai na burudani,” amesema.
Aidha, amesema maonyesho hayo yatakuwa na kaulimbiu isemayo “Biashara kijani uchumi na mazingira Endelevu” huku akisisitiza kuwa yanalenga kuchochea maendeleo ya uchumi na kuunganisha Tanzania na masoko ya kimataifa.