Tuungane pamoja tuimalize Morocco | Mwanaspoti

LEO ndiyo leo na asemaye kesho muongo, maana timu yetu ya taifa ‘Taifa Stars’ inaweza kuandika historia ya kibabe kwenye mashindano ya CHAN au safari yake ikaishia kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa itakapokabiliana na Morocco.

Na kwa vile ni robo fainali, maana yake timu itakayopoteza itaaga rasmi mashindano hayo yanayoshirikisha wachezaji wanaocheza ligi za ndani tu na itakayopata ushindi iwe kwa dakika 90, 120 au mikwaju ya penalti itasonga mbele.

Sisi hapa kijiweni tumekubaliana wote twende Uwanja wa Benjamin Mkapa kuiunga mkono Taifa Stars ili ipate ushindi katika mchezo huo na tuna sababu tatu za msingi tunazoamini zinatulazimisha kwenda kwa namba kubwa uwanjani ili kuwahamasisha wachezaji wetu.

Sababu ya kwanza ni kulinda heshima ya kucheza nyumbani. Siyo jambo zuri na ni aibu kwa mwenyeji kuondolewa mapema bila kuingia hatua ya nusu au fainali maana kitakachotokea baada ya kutolewa kinaweza kutukatisha tamaa na ladha ya kufuatilia mashindano hayo.

Lakini la pili ni kuthibitisha hatukuongoza kundi letu kwa kubahatisha au kwa sababu lilikuwa na timu nyepesi kama Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Kenya ‘Harambee Stars’, Benni McCarthy alivyoamua kutoa kauli ya kejeli tumeingia robo fainali kwa kukutana na timu nyepesi.

Tukimpiga Morocco itatujengea heshima kubwa, pia itawafanya hata wale wanaoamini tulikuwa kwenye kundi mchekea hatua iliyopita wajione walikuwa wanakosea kufikiria hilo.

Sababu ya tatu ni kuwasaidia wachezaji wetu kuandika historia katika mashindano haya ambayo itadumu vizazi vingi vijavyo na kuwafanya waingie katika orodha ya watu walioifanyia mambo makubwa nchi hii.

Hawa wachezaji wetu ni bora sana na wengi tayari wameshapata mafanikio makubwa barani Afrika wakiwa katika klabu zao hivyo wamebakiza fursa ya kufanya hivyo wakiwa na jezi za timu ya taifa jambo ambalo linaweza kufanyika sasa kupitia CHAN 2024.

Tumewasapoti wakiwa katika klabu zao na wakatuheshimisha hivyo tushirikiane kwa pamoja kuwaunga mkono wakiwa katika timu ya taifa hivi sasa kwani ni heshima kubwa kuacha alama ya kulipa heshima taifa.