Dar es Salaam. Katika dunia ya kisasa inayozidi kutawaliwa na teknolojia, simu janja na televisheni zimekuwa sehemu ya maisha ya kila siku kwa mamilioni ya watu duniani. Watu wanazitumia kwa kazi, mawasiliano, elimu, burudani, na hata kwa mahitaji ya kijamii.
Lakini pamoja na faida zake nyingi, vifaa hivi vina upande wa pili ambao mara nyingi hupuuzwa, nayo ni madhara ya kiafya yanayotokana na matumizi ya kupita kiasi ya vioo vyao.
Matatizo ya kiafya yanayohusishwa na matumizi haya yameongezeka kwa kasi, hususan miongoni mwa watoto, vijana, na hata watu wazima.
Uchovu wa macho, maumivu ya mgongo, usingizi hafifu na hata matatizo ya afya ya akili ni baadhi tu ya madhara yanayoendelea kuripotiwa.
“Teknolojia ni zawadi kubwa kwa binadamu, lakini kama haitatumika kwa kiasi, inaweza kuwa chanzo cha mateso ya kimya kimya,” anasema Dk Asha Msemo, mtaalamu wa magonjwa ya macho.
Wataalamu wa afya wanaonya kuwa kutazama vioo vya skrini kwa saa nyingi huongeza tatizo linalojulikana Kiingereza kwa jina la “Digital Eye Strain”, ambapo macho hukauka, huona ukungu au kuumia kutokana na kutopumzika.
Kadri mtu anavyotazama kioo cha vifaa hivyi, ndivyo anavyopunguza kupepesa macho, jambo linalopunguza unyevu asilia wa macho.
Zaidi ya hayo, watu wanaokaa kwa mikao isiyo sahihi wanapoitumia simu au kutazama runinga, huwa katika hatari ya kuathirika na maumivu ya shingo, mabega, na mgongo. Hali hii hujulikana kitaalamu kwa jina la “Text Neck Syndrome”.
Lakini si macho na mgongo tu vinavyoathirika. Matumizi ya simu usiku au kutazama runinga hadi usiku wa manane kunasababisha kuvurugika kwa mzunguko wa usingizi.
Mwanga wa bluu unaotolewa na vioo hivi huathiri utoaji wa homoni ya melatonin, ambayo ni muhimu katika kuleta usingizi. Hii husababisha uchovu wa kila mara, hasira bila sababu, na kushuka kwa kiwango cha umakini kazini au darasani.
Zaidi ya athari za kimwili, kuna pia athari kubwa za kisaikolojia. Tafiti mbalimbali zimeonyesha kuwa matumizi ya muda mrefu ya mitandao ya kijamii kupitia simu yamehusishwa na ongezeko la hali ya kutoridhika, kujilinganisha na wengine, wivu, msongo wa mawazo na hata unyogovu.
Vijana wengi wameingia katika hali ya kutengwa na jamii kwa sababu wanaishi zaidi maisha ya kidijitali kuliko maisha halisi.
Uwepo wa teknolojia umepunguza mwingiliano wa ana kwa ana, na kwa baadhi, hata uwezo wa kujieleza kwa ufasaha umepungua.
“Muda mwingine mtu ana marafiki elfu moja mtandaoni, lakini hana hata mmoja wa kweli wa kumtembelea wakati wa shida,”anaeleza
Juma Kambwili, mtaalamu wa mifumo ya kidijitali.
Pamoja na hayo yote, wataalamu wa afya wanashauri kuweka mipaka ya matumizi ya vifaa hivi. Shirika la Afya Duniani (WHO) linapendekeza kuwa watoto wenye umri wa miaka miwili au chini wasitazame kabisa vioo vya vifaa hivi, isipokuwa kwa mawasiliano ya video na familia.
Watoto wa miaka miwili hadi mitano wanapaswa kutumia si zaidi ya dakika 60 kwa siku, huku watoto wakubwa na watu wazima wakishauriwa kutumia simu au kutazama televisheni kwa saa mbili hadi tatu kwa siku tu, nje ya matumizi ya kielimu au kikazi.
Aidha, kuna kanuni rahisi inayojulikana kama “20-20-20” ambayo hupendekezwa: baada ya kila dakika 20 za kutazama skrini, mtu atazame kitu kilicho mita sita mbali kwa sekunde 20, ili kupumzisha macho.
Hata hivyo, haimaanishi kwamba vifaa hivi ni vibaya kwa kila hali. Zina faida kubwa pia. Simu na televisheni zimekuwa nyenzo muhimu ya elimu. Kupitia vipindi vya kielimu, watoto na watu wazima wameweza kujifunza mambo mapya kwa njia rahisi na ya kuvutia.
Zaidi ya elimu, simu na televisheni hutoa fursa ya burudani na kupunguza msongo wa mawazo. Michezo ya video, sinema, vipindi vya ucheshi na habari ni baadhi ya maudhui yanayosaidia watu kupumzika baada ya kazi au masomo.
Pia, vifaa hivi hurahisisha mawasiliano kati ya watu walioko mbali, kuwezesha kufanya biashara, mikutano ya kielektroniki, na hata kupata huduma za kiafya kwa njia ya mtandao.
“Si vifaa vinavyotuumiza, bali ni namna tunavyovitumia. Simu ni rafiki bora ikiwa utaweka mipaka,”anasema Neema Mbuya, mshauri wa afya ya jamii
Hii inatuonyesha kuwa suluhisho si kuachana kabisa na teknolojia, bali ni kuwa na matumizi yenye mipaka. Tunapaswa kujenga tabia ya kuweka muda maalum wa kutumia simu na runinga, kuchagua maudhui bora, na kuhakikisha tunatoa nafasi kwa shughuli za kijamii, michezo, mazoezi na mawasiliano ya ana kwa ana.
Vilevile, wazazi wanapaswa kuwa mfano kwa watoto wao kwa kupunguza matumizi ya simu nyumbani, kuweka sheria za familia kuhusu muda wa kutazama televisheni au kutumia simu, na kushiriki shughuli mbadala kama kusoma vitabu pamoja, kuzungumza au kushiriki michezo.