Dar es Salaam. Wakati nchi ikielekea kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia, wadau wameshauri Shirika la Viwango Tanzania (TBS) liwe na mfumo maalumu wa ukaguzi, ili kubaini vifaa vya kielektroniki vya kupikia visivyo na ubora.
Wito huo umefuatia malalamiko kadhaa kutoka kwa watumiaji ambao walipata changamoto ya vifaa hivyo kuharibika mapema, kutokana na kukosa ubora.
Hayo yamesemwa leo Ijumaa, Agosti 22, 2025 wakati wa Kongamano la Pika Kijanja 2025 lililoandaliwa na Bongo FM, lililojadili namna ya kufikia malengo ya asilimia 80 ya Watanzania wanaotumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.
Mwakilishi wa Mradi huduma za kisasa za kupikia (MECS), uliopo chini ya Shirika la Maendeleo la Uingereza UKAID, Charles Barnabas amesema urahisi na nafuu ya gharama katika nishati zote za kupikia vipo kwenye umeme, ingawa kuna vikwazo hasa vya ubora wa vifaa.

“Kuna kikwazo cha viwango, TBS hawana mifumo ya kugundua vifaa vya kupikia vya umeme ambavyo ni imara, majiko yanayotumia umeme yanayotengenezwa mengi hayana ubora, wananchi wananunua lakini wakienda kutumia muda mfupi yameharibika,” amesema Barnabas.
Pia, ametaja elimu akinyooshea kidole dhana ya kwamba wanaotumia umeme ni watu wa maisha yenye hadhi fulani au iliyonyanyuka kiuchumi na pia hawatumii gesi wakidhani si saizi yao.
Hata hivyo, amesema vikwazo vingine vinavyotakiwa kushughulikiwa, ni uwepo wa mafundi ili yakiharibika wanakwenda kutengeneza, ni eneo ambalo bado kuna changamoto.
“Inatakiwa wawepo mafundi maalumu ambao wataweza kuwasaidia wananchi pindi wapatapo changamoto,” amesema.
Barnabas ametaja kikwazo kingine kuwa ni imani potofu kuhusu chakula kilichopikwa kwenye kuni au mkaa, kwamba si sawa na kilichopikwa katika gesi au jiko la umeme.
“MECS tumewahi kufanya utafiti, tulipika wali, pilau kwenye kuni, mkaa, gesi na tukawapa wagonjwa waseme vyakula hivyo vimepikwa kwa nishati ipi, zaidi ya asilimia 90 ya wahudhuriaji walishindwa kujua kimepikwa kwa nishati ipi, hivyo si kweli wali wa kwenye mkaa ni bora kuliko gesi au umeme,” amesema.
Dhana hiyo inaelezwa na mtaalamu wa saikolojia, Deo Sukambi kuwa kikwazo kikubwa katika jamii na kwamba hilo ni suala la kisaikolojia.
“Kwa mtoto aliyezoeshwa wali uliopikwa na kuni kwa sababu ndio ufahamu wake, anaamini hivyo wakati si kweli, bali ni tafsiri yake tu.
“Ni wakati sasa kuanza kupambana na imani potofu, utamu unapatikanaje? Ni mapishi na mawazo ya kichwani, yupo aliyezaliwa wali unapikwa kwenye rice cooker na ni mtamu, akila wa kuni au mkaa atahisi tofauti sababu ya imani tu.”
Kwa mujibu wa Sukambi, kipengele cha saikolojia ni muhimu na ndicho kinachochukua maamuzi ya mtu.

Amesema lazima jamii ishirikishwe, kwa ukali haitasaidia na kwa upole haitasaidia, ila waambiwe si ujanja kupikia kuni na mkaa, waelezwe madhara na faida za kutumia nishati safi ya kupikia.
“Waelezwe manufaa ya kijamii, kiroho na manufaa ya kiuchumi wajue kutumia nishati safi wanaokoa kiasi gani, wanapunguza gharama ngapi, wanajiepusha na madhila mangapi,” amesema Sukambi.
Katika uzinduzi wa kongamano hilo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema msukumo wa Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu nishati safi unalenga kuboresha afya na thamani ya mwanamke na mwanaume kwa manufaa ya taifa.
“Matumizi ya nishati safi kupikia tuanze sasa, tusipoanza sasa miaka kadhaa baadaye miti itaisha mvua isiponyesha, Dar una hela mkononi na chakula cha kununua hakuna, na aliye kijijini hana chakula, hana hela,” amesema Chalamila.
Amesisitiza umuhimu wa kuanza kutumia nishati safi sasa ili kupunguza uharibifu wa mazingira na kupanda kwa gharama za maisha siku zijazo.
Mkurugenzi wa Tamwa, Dk Rose Reuben, amesema wanawake na watoto ndio wanaoathirika zaidi na nishati duni ya kupikia, hivyo usawa wa kijinsia na ushirikiano wa jamii nzima ni muhimu.
Amesisitiza vyombo vya habari kutumia nafasi yao kuongeza uelewa ili kufikia lengo la asilimia 80 kutumia nishati safi.
Kamishna wa Nishati Jadidifu, Innocent Luoga, amesema wizara imeanza utekelezaji tangu mwaka 2022 kwa kusambaza mitungi ya gesi kwa mamalishe na babalishe. Mpango huo ni sehemu ya agizo la Rais Samia na unalenga kuwainua wanawake barani Afrika.
Kwa upande wake, Emmanuel Muro wa UNCDF alisema wanatoa mitaji na ruzuku kwa kampuni zinazouza bidhaa za nishati safi, ili kupunguza gharama na kufikisha huduma vijijini.
Awali, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Daphrosa Kimbory, amesema lengo la kongamano ni kuongeza hamasa na elimu kuhusu nishati safi.