Morogoro. Tathmini ya mapambano dhidi ya udumavu na upungufu wa lishe bora hasa kwa watoto chini ya miaka mitano na wajawazito, imebaini uwepo wa changamoto kadhaa ikiwamo uelewa mdogo wa wazazi na walezi.
Hayo yamebainika katika kikao cha viongozi wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara, wataalamu kutoka sekta mbalimbali pamoja na wadau wa lishe kuhusu tathmini ya nusu mwaka wa utekelezaji wa mkataba wa lishe kwa kipindi cha Julai 2024-Juni 2025 kilichofanyika leo Mkuu wa Wilaya ya , Dunstan Kyobya akiwa mgeni rasmi na mwenyekiti wa kikao.
Changamoto zilizobainika ni uhitaji wa nguvu ikiwemo uelewa mdogo wa wananchi hususani wazazi na walezi wa wanafunzi kuhusu matumizi ya vyakula vyenye virutubisho, ukosefu wa rasilimali za kutosha na changamoto za kiafya zinazochangia udumavu.
Akizungumza kwenye kikao hicho Mkuu wa Wilaya Kyobya amesema kuwa bado kuna changamoto kubwa kwa wazazi na walezi wa wanafunzi kuchangia lishe shuleni.
Kyobya amesisitiza mshikamano kwenye sekta zote, na kusema kuwa mapambano ya lishe si jukumu la sekta ya afya pekee, bali yanahitaji ushiriki wa kilimo, elimu, maji na jamii kwa ujumla.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara, Pilly Kitwana amewahimiza wataalamu na wadau kuongeza ubunifu na mikakati ya kuhakikisha wananchi wanapata lishe bora kupitia uzalishaji na matumizi ya nishati, barabara, maji pamoja na mazao yanayopatikana ndani ya jamii.
Miongoni mwa mada zilizowasilishwa na wataalamu ni taarifa iliyoonesha maendeleo yaliyofikiwa katika kutoa elimu ya lishe kwa jamii, upatikanaji wa chakula bora na utekelezaji wa miradi ya kuongeza kipato kwa kaya.
Kutokana na changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii ya Ifakara katika eneo la lishe, baadhi ya wadau wameamua kuchukua hatua madhubuti kwa kuimarisha ushirikiano wao.
Ushirikiano huu unalenga kuhakikisha afua za lishe zinatekelezwa kikamilifu na kufuatiliwa kwa karibu ili kubaini mafanikio na changamoto zinazojitokeza.
Aidha, juhudi hizo zinajumuisha kupeleka elimu ya lishe kwa wananchi wote, kwa lengo la kuongeza uelewa kuhusu mlo bora na umuhimu wa lishe sahihi kwa afya. Hatua hii inalenga kupunguza viwango vya udumavu kwa watoto na kuimarisha afya ya jamii kwa ujumla, sambamba na kukuza maendeleo endelevu katika eneo la Ifakara.