Arumeru. Wananchi zaidi ya 14,000 wa Kata ya Bwawani wilayani Arumeru mkoa wa Arusha, wameondokana na adha ya kufuata huduma ya afya umbali mrefu na kupelekea wagonjwa wengine kupoteza maisha njiani, baada ya kukamilika kwa ujenzi wa Kituo cha Afya Songambele.
Kituo hicho kilichogharimu zaidi ya Sh649.8 milioni kimejengwa na Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf), ambapo wananchi wa Kata hiyo walikuwa wakifuata huduma ya afya umbali wa kilomita 15, katika kituo cha afya Nduruma.
Akizungumza leo Ijumaa Agosti 22, 2025 katika ziara ya wadau mbalimbali wa maendeleo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Themi ya Simba kilipojengwa kituo hicho, Musa Msengi amesema kabla ya kumalizika kwa kituo hicho kina mama na watoto walikuwa wakiteseka kufuata huduma mbali.
“Tunashukuru ujenzi wa kituo hiki umetuondolea adha ya kwenda umbali mrefu kufuata huduma za afya, changamoto ilikuwa zaidi kwa akina mama na watoto, tunaamini kupitia kituo hiki hakutakuwa na vifo vitokanavyo na kufuata huduma mbali,” amesema.
Mmoja wa wananchi hao, Christina Jonas amesema mradi huo pamoja na miradi mingine ya uwezeshaji kiuchumi, imekuwa mkombozi wa jamii na kuwa awali wanawake wajawazito walikuwa wakiteseka kufuata huduma ya afya Kituo cha afya Nduruma.
“Kwa sasa tumeondokana na adha ya kutembea mbali kufuata huduma za afya, tunatibiwa hapa karibu kwa kweli inatusaidia, tumeinuka kiuchumi tumeweza kuanzisha miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo inatuongezea kipato cha familia,”
Akizungumzia mradi huo, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Bwawani, Simon Kaaya amesema Kata hiyo kupitia ufadhili wa OPEC katika mradi wa kupunguza umaskini Tanzania awamu ya nne, imetekeleza miradi mitano ambayo ni ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje, maabara, jengo la upasuaji, wodi ya akina mama na nyumba ya watumishi.
“Mradi huu utahudumia vijiji vyote vinne vya kata hii, kusogezwa huduma karibu na wananchi kwani walikuwa wakifuata huduma mbali hata kupelekea wagonjwa wengine kupoteza maisha njiani,” amesema.
“Katika mradi huu Tasaf imetoa Sh604.5 milioni na michango ya wananchi ikiwemo fedha taslimu, nguvu kazi, kubeba zana za ujenzi ikiwa zaidi ya Sh45.3milioni,” ameongeza.
Mkurugenzi wa Mifumo, Tafiti na Mawasiliano kutoka Tasaf, Japhet Boaz amesema lengo la ziara hiyo ni kukagua miradi inayotekelezwa kwa walengwa na kuwa matokeo ya awali ya mradi huo yanaonyesha mradi umefanya vizuri na kuwa hadi Julai 2024, kaya zaidi laki nne kutoka kaya milioni 1.3 kote nchini zimehitimu na kuvuka kutoka kwenye umaskini na kujiweza.
Mwakilishi kutoka Umoja wa Ulaya (EU), Rebeca Sundbom amesema wamekuwa wakipita katika maeneo mbalimbali inakotekelezwa miradi ili kuona namna imefanya kazi na kubadili maisha ya walengwa.
“Lengo ni kuona namna miradi imenufaisha walengwa na maisha yao yalivyobadilika, tumejionea hapa kwa mfano huduma za afya ni kati ya huduma muhimu kwa jamii ambayo inapaswa kuwa karibu na wananchi hivyo kusogezwa kwa huduma hii karibu ni jambo lenye manufaa makubwa,” amesema.